×

Kituo cha afya Mbagala chalalamikiwa

DSC00585Kituo cha Afya cha Mbagala Rangi Tatu kilichopo wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, baadhi ya watumishi wake wamelalamikiwa kwa kutumia lugha chafu kwa wagonjwa wanaokwenda kutibiwa.

Wakizungumza na mwandishi wetu, baadhi ya wagonjwa walidai kuwa baadhi ya manesi kituoni hapo wamekuwa na lugha chafu kwa wagonjwa na hata huduma wanazopata, wanatoa kwa kujilazimisha.

Mgonjwa mmoja wa Kifua Kikuu (jina linahifadhiwa) alisema alikwenda katika kituo hicho akiwa na hali mbaya sana lakini alipofika na kuomba tiba ya sindano kama alivyoandikiwa na daktari badala ya kuhudumiwa, alijibiwa maneno mabaya na akajisikia vibaya.

“Inashangaza sana. Baadhi ya watumishi katika kituo hiki cha afya hawana wito na kazi yao, walinijibu vibaya sana nilipokwenda kupata sindano ya TB (Kifua Kikuu),” alilalamika mgonjwa huyo.

Mama mwingine (jina tunalihifadhi) alilalamikia huduma za wajawazito akidai kuwa baadhi ya manesi wana lugha chafu kwa akina mama wanaokwenda kwa lengo la kujifungua.

“Kuna wakati inatulazimu kwenda kupata huduma hii katika hospitali zingine kukwepa kero za hapa Kituo cha Mbagala, pale ukiwa na Bima ya Afya ndiyo manyanyaso yanazidi, huthaminiwi,” alidai mama huyo.
Mganga mfawidhi wa kituo hicho, Dk. Joseph Kiani alipoulizwa juu ya madai hayo alisema malalamiko hayo hayajamfikia na aliwataka wagonjwa wenye malalamiko kwenda chumba namba moja ambacho hushughulikia kero zote.

Naye Msemaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Joyce Msumba alipoulizwa alisema: “Mganga mkuu wilayani hana taarifa hizo. Aliwataka wagonjwa wote wenye kero kuonana na uongozi wa kituo hicho cha afya haraka iwezekanavyo.”

Leave a Comment