×

Kumficha mkeo mshahara wako ni ujinga au ujanja?

love, family, finance, money and happiness concpet - smiling couple with money and piggybank ot table at homeNinachokifahamu mimi ni kwamba, watu wawili waliotokea kupendana wanapoamua kuingia kwenye ndoa, wamekubali kuwa mwili mmoja. Hii ina maana kwamba, mke na mume hawawezi kufichana kwa lolote.

Yapo mambo mengi ambayo najua hata wewe msomaji huwezi kumwambia mtu mwingine yeyote lakini mkeo/mumeo utampa ukweli ukijua amekuwa ni sehemu ya mwili wako.

Licha ya ukweli huo, najua wapo ambao wameoana lakini maisha yao ni kama vile wako kwenye hatua ya uchumba. Ule umoja kwa maana halisi ya umoja hakuna, kila mmoja anafanya mambo yake vile anavyojisikia bila hata kumshirikisha mwenzake.

Hali huwa mbaya zaidi pale ambapo mtaoana mkiwa wote mnafanya kazi halafu wote au mmoja wenu anakuwa mbinafsi. Kwa kifupi ndani ya ndoa nyingi unazoziona kuna siri nzito.

Hata hivyo, kitu ambacho nataka kukizungumzia leo ni kuhusu hii tabia ya baadhi ya wanandoa kutokuambiana ukweli juu ya mishahara yao. Tabia hii wamekuwa nayo wanaume wengi licha ya kwamba wapo baadhi ya wanawake walioajiriwa nao wamekuwa wagumu kuweka wazi mishahara wanayopata.

Sikatai ni uamuzi wako kuweka wazi kila kitu kwa mwenza wako au kumficha baadhi ya mambo kwa sababu unazozijua lakini unadhani unaposema wewe na mkeo ni mwili mmoja halafu ukawa bado unamficha baadhi ya mambo utakuwa unafanya sawa?

 Unadhani ni ujanja kuwa unapokea mshahara kwa mfano wa milioni moja halafu mkeo ukamwambia unapokea laki 5? Sawa, unaweza kuwa na sababu ya kufanya hivyo lakini nikuulize ni sababu gani ambazo mkeo hatakiwi kuzijua?

 Mbaya zaidi wengine siyo kwamba wana sababu za msingi bali lengo lao mshahara ujulikane ni nusu ya kile anachokipata ili nusu nyingine aifanyie mambo yake (ikiwemo starehe). Sasa hapo utakuwa unamkomoa nani?

 Wakati f’lani niliwahi kuzungumza na mwanasaikolojia maarufu jijini Dar, akaniambia kuwa ili niweze kupata mafanikio kwenye maisha yangu nisimfiche mke wangu kwenye suala lolote linalohusu pesa.

Akaniambia kuwa, wanawake wengi wako smati sana kwenye pesa, unapokuwa muwazi kwenye mshahara unaopata ni rahisi sana kukusaidia ‘kuukontroo’ na ukafanyia mambo ya kimaendeleo.

Akaniambia nikiwa napokea kwa mfano laki moja, kisha nikasema napokea 50,000 ni rahisi sana ile hamsini nyingine kuifanyia mambo ya kipuuzi. Mimi nafuata ushauri wake na matokeo nayaona.

 Hivyo basi, mimi sikuelekezi uishije na mkeo linapokuja suala la pesa lakini ni vyema ukajua kwamba, unapokuwa muwazi kwa mkeo ni rahisi sana kuzitumia pesa kwenye mambo ya msingi. Asikudanganye mtu, wanawake wengi wana nidhamu ya pesa kuliko waume zao, ndiyo maana baadhi ya familia zimekuwa na mafanikio makubwa baada ya wanaume kuwageuza wake zao wahasibu.

Unaweza kuwa unapokea mshahara mdogo lakini utakapomshirikisha mkeo utashangaa mnafanya mambo makubwa kuliko hata yule ambaye anachukua mshahara mkubwa.

Wapo wanaume ambao wakipokea mshahara, moja kwa moja hadi kwa wake zao. Wale siyo wajinga, wanajijua wakibaki nazo mifukoni zitayeyuka bila kufanya mambo ya msingi.

Kwa maana hiyo sasa, leo niseme tu kwamba kumficha mkeo au mumeo mshahara wako wala siyo ujanja. Kumbuka huyo ni mkeo, sasa kama umejenga imani naye, ukaamini ni mwanamke mwerevu, anayeweza kutoa uamuzi sahihi kuhusu pesa unayopata kwa nini umfiche?

Pia niwaseme na wale wake za watu wenye tabia ya kutotaka waume zao wajue mishahara yao. Watu hao huenda mbele zaidi kwa kufanya mambo yao kwa siri wakitumia mishahara yao.

 Niseme tu kwamba hiyo tabia siyo nzuri na naahidi katika makala zijazo nitawazungumzia kwa kirefu wanawake hao.

KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

*********

JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

ERIC SHIGONGO INSTAGRAM: @ericshigongo

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: Global TV Online

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE:@shigongotz

Leave a Comment