MUHAMMAD Ali, bingwa wa dunia wa uzito wa juu mara tatu, amefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 74, kwa ugonjwa wa muda mrefu wa Parkinson.
Parkinson ni ugonjwa unaotokana na athari katika mfumo wa fahamu na madhara yake yanaonekana kwa mgonjwa kutetemeka, kutokuwa na kasi katika kutembea, kuzungumza na mengine yanayofanana na hayo.
The Greatest, kama alivyofahamika kutokana na uwezo wake wa kuzichapa, amefariki akiweka rekodi ya kuwa bondia aliyekuwa na uwezo wa hali ya juu ulingoni, lakini pia akiwa na roho nzuri mno nje ya ulingo.
Ali, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Cassius Marcellus Clay Jr, alipigana ngumi katika kipindi ambacho dunia ilishuhudia mabondia wengi mahiri, waliokuwa na uwezo mkubwa wa kutupa makonde, lakini wote wakiangukia pua walipokutana na bondia huyo aliyehama Ukristo na kuingia Uislamu.
Historia inaonesha Ali, aliyezaliwa Januari 17, 1942, huko Louisville, alijifunza ngumi akiwa na umri wa miaka 12, baada ya watu wasiojulikana, kumuibia baiskeli yake na alipokwenda polisi kushtaki, ofisa aliyemkuta akamshauri kujifunza ubondia ili akijua, amchape vizuri mwizi wake. Alijifunza na kupanda ngazi hadi kuja kuwa mwenye sura inayojulikana zaidi duniani, hasa alipokuwa katika kilele cha ubora wake miaka ile ya 1970.
Alisifika kwa mbinu zake za kuwakejeli wapinzani na kutoa misemo iliyopeleka ujumbe wa vitisho kama wakati mmoja alipomuita mpinzani wake, Sonny Liston kuwa ni Dubu Mwenye Sura Mbaya.
Lakini jina baya zaidi kuwahi kulitoa ni pale alipomuita mpinzani wake mkubwa ulingoni, Joe Frazier kuwa ni sokwe, baada ya kuwa awali alimbatiza kama Uncle Tom.
Ali alipigana na mpinzani wake huyo mara kadhaa, lakini pambano lao lililoweka historia, ni lile lililopigwa Manila nchini Philippines, Oktoba 1, 1975. Katika mkutano mmoja na waandishi wa habari, bondia huyo alitoa picha ya sokwe mfukoni na kuanza kuipiga ngumi huku akimponda.
Frazier, alichukia sana kwa kitendo hicho na kwa zaidi ya muongo mmoja baadaye, aliishi akiwa na chuki dhidi ya bondia huyo.
Hata hivyo, kabla ya kifo cha Frazier mwaka 2011, aliwahi kuhudhuria hafla moja ya kimichezo huko Las Vegas. Frazier alichukua kopi ya gazeti la michezo la zamani ambalo lilikuwa na picha yake na Muhammad Ali wakiwa na promota Don King katika ukurasa wa kwanza.
“Mzee, mimi na Ali tuliwapa watu kumbukumbu nzuri sana,” maneno yaliyoashiria kuondoka kwa kinyongo chake dhidi yake.
Ali aliwapiga wengi katika ubora wake kama Zora Folley pale New York, Machi 22, 1967. Baada ya pambano, mkali huyo alisema hakuwa amewahi kukutana na bondia anayejua ngumi kama Ali na kwamba kwa uwezo wake, anaweza kuandika kitabu kizuri kuhusu ngumi na kingeuza.
Aliingia katika mgogoro na serikali ya Marekani baada ya kukataa kujiunga na jeshi ili kwenda kupigana katika vita vya Vietnam na alibadili dini mwaka 1964 baada ya ushindi wake dhidi ya Liston.
Mapambano mengine ya kukumbukwa ya shujaa huyo ni lile dhidi ya George Foreman ambalo lilipigwa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo) mwaka 1974 na lile la mwaka 1980, dhidi ya Larry Holmes.
Kumbukumbu nyingine ya bondia huyo ni kukataa kwake kusema ni nani anamuunga mkono katika uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 1976, kati ya Gerald Ford wa Republican na Jimmy Carter wa Democrat, kwa kile alichosema kuepuka kuwafanya wafuasi wake kumpigia kura atakayemtaja, wakati huo ni uamuzi binafsi wa mtu.
