MCHEZO wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika mwakani nchini Gabon uliozikutanisha Taifa Stars na Misri, umeleta balaa baada ya ndugu wawili kuzozana na hatimaye kutokea mauaji.
Mchezo huo uliopigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, ulimalizika kwa Stars kufungwa mabao 2-0 na kufuta ndoto za kufuzu michuano hiyo.
Ishu ilikuwa hivi; ndugu wawili waliofahamika kwa jina mojamoja la Juma na Adamu wakazi wa Mtaa wa Gogo Kata ya Zingiziwa, Chanika, waliokuwa wakiushuhudia mchezo huo kwa njia ya runinga, waliingia kwenye ubishi uliogharimu maisha ya Juma.
Inaelezwa kuwa ubishi wao ulianza baada ya mshambuliaji wa Stars Mbwana Samatta kukosa penalti kwenye mchezo huo, huku mmoja akimtetea Samatta na mwingine akimponda.
Mashuhuda wa tukio hilo, wamesema wakati wakiushuhudia mchezo huo huku ubishani ukiendelea, ghafla Adamu akamchoma kisu Juma hali iliyozua taharuki eneo hilo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, mwenyekiti wa mtaa huo, Ramadhan Mapunda, amesema: “Ni kweli tukio hilo limetokea jana (juzi) kwenye mtaa wangu, kuna kijana mmoja anaitwa Juma ameuawa na kaka yake anayeitwa Adamu, hao vijana walikuwa kwenye ubishani wa masuala ya mpira, inaonekana kwamba Juma alitoa neno ambalo halikumpendeza Adamu.
“Hawa wote ni wafanyabiashara wanaouza nyama, sasa wakati mabishano hayo yakiendelea, bila ya kutarajia Adamu akaingia katika duka la nyama akatoka na kisu na kumchoma ndugu yake huyo tumboni, akaanguka chini. “Baada ya hapo watu waliokuwa pale wakamchukua Juma ili kumuwahisha hospitali akapate matibabu, lakini baada ya kufika kwenye Kituo Kidogo cha Polisi Chanika kwa ajili ya kuchukua PF3, Juma akafariki na wakati huo Adamu alifika kituoni hapo, hivyo ikawa rahisi kwa polisi kumkamata na kumuweka ndani akituhumiwa kwa mauaji.”
Mmoja wa maafande wa kituo hicho cha polisi ambaye hakupenda kutaja jina lake kutokana na kwamba siyo msemaji mkuu wa ishu hiyo, alisema ni kweli mtu huyo alikuwa kituoni hapo lakini kutokana na kituo chao hicho kuwa kidogo, wakamuhamishia Kituo cha Polisi Stakishari.
