×

Mwenge wa Uhuru wachoma madawa ya kulevya

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2016 akiwa na     kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Songea wakiteketeza dawa za     kulevya Lizabon Songea mjiniStephano Mango, Amani

RUVUMA: Vita imepamba moto! Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2016, George Mbijima akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Songea wameteketeza madawa ya kulevya ‘unga’ kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Mloweka mjini Songea (pichani)yaliyokamatwa na polisi katika manispaa hiyo, mwaka huu, tembea na Amani.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Benson Mpesya katika risala ya utii kwa rais wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Juni 8, mwaka huu alibainisha kuwa, katika kukabiliana na ‘unga’ elimu sahihi inatolewa kwa vijana ili wajiepushe na matumizi yake na kuwafichua wote wanaouza na kulima.

mwengeAliongeza kuwa, kupitia mfumo wa polisi jamii wananchi wengi wamejitokeza kuwafichua wanaojishughulisha na biashara hiyo ambapo msako wa kuwakamata unafanyika katika mitaa yote mjini Songea.

Utafiti umebaini kuwa, matumizi ya madawa ya kulevya  hasa kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 45 bado ni tatizo kubwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Naye Ofisa Habari wa Manispaa ya Songea, Albano Midelo alisema takwimu zinaonesha kuwa, katika kipindi cha mwaka 2015, manispaa hiyo ilikuwa na waathirika wa unga 145 kati ya hao, wanaume ni 138 na wanawake 7.

Alisema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Mei, 2016, Manispaa ya Songea ina  jumla ya waathirika wa unga 97, kati yao wanawake wawili na wanaume  95 ambapo waathirika wote wakiwa na umri kati ya miaka 15 hadi 45.

Kutokana na hali hiyo, alitoa rai kwa wadau kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya madawa ya kulevya ili kujenga  jamii na maisha na utu wa mtu bila matumizi jambo ambalo ni tatizo si kwa manispaa hiyo bali kwa vijana nchini kote.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea, Dk. Simon Chacha alisisitiza kuwa, kuongezeka kwa tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya inadhihirishwa na kuwepo kwa waathirika wake mitaani na wale wanaofika hospitalini wakiwa hawajiwezi.

Hata hivyo, alisema kutokana na athari hiyo, ametoa wito kwa vijana na kwa wananchi wote kutojihusisha kwa namna yoyote katika matumizi ya unga. Pia aliwashauri walioathirika kwenda kwenye vituo vya afya kupata tiba na ushauri.

Leave a Comment