×

Malima: Nataka Kuleta Mapinduzi Bongo Muvi

Director Malima

Director Malima.

Na Leonard Msigwa/GPL

DAR ES SAALAM: Soko la filamu nchini “Bongo Muvi” limepata muongoza filamu “director” mpya na anayechipukia kwa kasi ambaye anajulikana kwa jina la John Christopher Malima (21), maarufu kwa jina la Director Malima ambaye ni muongoza filamu aliyejikita kwenye kuongoza na kutengeneza filamu za mapigano kama ambavyo waongozaji waliopo nchi nyingi zilizoendelea duniani wanafanya.

Director Malima mwenye makazi yake jijini Dar es Saalam akiishi mtaa wa Kimara Suka, amesema ameingia kwenye ulimwengu wa filamu nchini kwa lengo moja tu kuleta mapinduzi kwenye tasinia hiyo ambayo kwa miaka ya hivi karibuni inaonekana kuporomoka.

Msanii huyo amezungumza mengi alipofanya mahojiano na Global Digital na kusema:

“Nimeamua kuingia kwenye tasnia hii ya filamu nchini ili nami nichangie mawazo yangu ili kwa pamoja tuweze kuibadili tasinia hii ya filamu nchini na iweze kushindana na filamu zinazotayarishwa sehemu nyingine duniani kama Marekani na hata India pia.

“Filamu zangu zitajikita zaidi kwenye mapigano, yaani nitaongoza na kusimamia filamu zenye mapigano ndani yake kama zile za akina Jean Claude Van Dame, Dolph Lundgren na Sylvester Stallone ‘Rambo’  ambazo huwa tunaaminishwa kwamba ni kweli japokuwa siri hii tunayo waongozaji.

“Tayari nimesimamia na kuongoza filamu kadhaa za kivita ambazo naamini zitafanya vyema sokoni na kuleta ladha mpya kwenye soko la filamu nchini. Lazima tuongeze ubunifu zaidi ili soko letu la filamu nchini liweze kukua na kuweka ushindani kwenye soko la kimataifa.

“Mwezi Disemba ndiyo nitatoa filamu yangu ya kwanza nawaomba mashabiki wangu wakae mkao wa kula naamini filamu hiyo italeta mapinduzi makubwa na itakidhi mahitaji ya watazamaji wangu.

Alipobanwa na Global Digital amesomea wapi utaalamu huo, Malima amesema:

“Nilianza kujifunza nikiwa mdogo kupitia kwa shemeji yangu ambaye ni raia wa nchini Uingereza, baadae niliacha kazi yangu ya u-dj na kuamua kujikita kwenye kitengo hiki hadi mwaka 2013 ndipo niliweza kuandaa mwenyewe kila kitu kwenye filamu za mapigano na tangu wakati huo natengeneza na kusimamia mwenyewe filamu za mapigano.

1 Comment

Leave a Comment