
Ambene Yesaya ‘AY’.
Makala: Gabriel Ng’osha
KWA mara ya kwanza tangu amuanike katika mitandao ya kijamii mchumba wake anayejulikana kwa jina moja la Remy, mkongwe wa Muziki wa Bongo Fleva, Ambwene Yessaya ‘AY’ amefichua alivyompata ilitokana na kumpenda msanii wa Nigeria, Helen Folasede Adu ‘Sade Adu au Sade ambaye anafanana naye kwa asilimia kubwa.
Akizungumza na Over Ze Weekend, AY anayebamba kwa sasa na Ngoma ya More n More aliomshirikisha Nyashinski kutoka Kenya alisema kuwa, Sade ni mwanamuziki aliyemvutia kwa muda mrefu na kumfanya atafute mwanamke anayefanana naye.
Katika makala haya, AY amefunguka zaidi kuhusu uhusiano wake;
Mpenzi wa AY, Rmmy.
Over Ze Weekend: Tungependa kujua lini ulimfahamu Sade?
AY: Nimeanza kumfahamu Sade tangu nikiwa mdogo ila kupitia nyimbo zake ambazo marehemu baba yangu alikuwa anapenda kuzisikiliza, tangu hapo nilianza kumpenda.
Over Ze Weekend: Nini hasa kilichokuvutia kwake kiasi cha kutamani kupata mwanamke mwenye sifa zake?
AY: Ni kati ya wanamuziki wachache duniani wanaopendwa sana, anafanya vitu kwa kufikiria na ndiyo maana kazi zake zinadumu na hata muonekano wake ni mzuri, ni mrembo sana, hazeeki na hana skendo za ajabuajabu kama wengine. Kingine wanamuziki kama Dr Dre, Mr Chicks, Jay Cole, Jay Z wanamkubali sana. Nakumbuka rapa, Snoop Dogg aliwahi kusema kabisa kuwa, siku akifanya kolabo na Sade basi anastaafu kufanya muziki.
Over Ze Weekend: Umeshawahi kushirikiana au una mpango wowote wa kufanya naye ngoma yoyote?
AY: Duh! Kiukweli sina hata wazo hilo kwa sababu najua ni ngumu, ninaamini wasanii wakubwa kibao wanatamani kufanya naye ngoma.
Over Ze Weekend: Imekuchukua muda gani kumtafuta mwanamke mwenye tabia na sifa za Sade?
AY: Ni kama miaka minne hivi tumefahamiana, lakini haimaanishi kuwa ilikuwa ni lazima awe na sifa zote za Sade ndiyo awe na AY, sema ninachoshukuru ni kweli ana baadhi ya vitu anafanana naye.
Over Ze Weekend: Usingempata mchumba mwenye sifa za Sade, ungekuwa tayari kuwa naye katika uhusiano?
AY: Yah! Inategemea na jinsi ambavyo watu wana-link, haizuii lakini imetokea tu bahati kuwa na uhusiano na mtu ambaye anafanana naye, nimegundua kuwa ni mtu ambaye wamezaliwa kipindi kimoja, hicho kimenifurahisha pia.
Over Ze Weekend: Unaweza kututajia jina kamili la mpenzi wako?

Remy na Ay.
AY: Naomba nimtaje kwa jina moja tu la Remy siyo mtu wa media sana kwa hiyo sipendi kumuanika. Anajifahamu kuwa ana sifa za Sade na anampenda kwa hiyo wote ni wapenzi wa kweli wa Sade.
Over Ze Weekend: Unazungumziaje kuwa naye katika uhusiano ukiwa kama staa unayepata changamoto za kupendwa na wasichana wengi?
AY: Kwa muda ambao tumekuwa kwenye uhusiano ananifahamu tabia zangu na mwenendo wangu hivyo ananiamini nami namwamini.
Over Ze Weekend: Lini unatarajia kufunga ndoa au kumtambulisha kwa ndugu zako?
AY:Mungu ndiye hupanga kila jambo naamini muda ukifika kila kitu kitakuwa sawa.
Over Ze Weekend: Umetumia vigezo vipi katika kujiridhisha kuwa mchumba wako ana sifa za Sade?
AY: Muonekano, tabia na pia yeye mwenyewe anampenda sana Sade kwa hiyo wote tunamkubali na kumpenda Sade.
Over Ze Weekend: Je, Sade mwenyewe anafahamu kama una mahaba ya dhati kwake?
AY: Naamini hafahamu kwa sababu sijawahi kuonana naye ila nakumbuka niliwahi kuwasiliana na uongozi wake na walinitumia albamu yake ila ilipotea katika mazingira ya kushangaza, nawalaani sana walioichukua ingawa kuna wakati nilikuwa nawasiliana na mtoto wake.
Over Ze Weekend: Ukipewa nafasi ya kumfanyia jambo au kitu Sade, utamfanyia nini kutokana na kuwa na mahaba naye ya kweli?
AY: Nitamkaribisha Tanzania na kumtembeza ili aone uzuri wa Tanzania, nitampatia ‘collection’ ya nyimbo zangu na mambo mengine mazuri ambayo yanaweza kumpendeza mtu yeyote.

Helen Folasede Adu ‘Sade Adu ‘SADE’
SADE NI NANI? Ni mwanamuziki kutoka jamii ya Wayoruba, aliyezaliwa mwaka 1959, Ibadan katika Jimbo la Oyo nchini Nigeria ambaye mama yake ni raia wa Uingereza nafasi ambayo ilimuwezesha kuishi na kupewa uraia wa nchi hiyo. Akiwa na Bendi ya Sade amefanikiwa kuachia album kibao ikiwemo Diamond Life (1984), Absolute Beginners (1986), Stronger Than Pride (1988) and Love Deluxe (1992) Lovers Rock (2000), Soldier of Love (2010) na nyingine kibao. Sade pia anatambulika kama Mwanamuziki Bora wa Solo wenye Mafanikio nchini Uingereza. Sade amewahi kuteuliwa kuwania tuzo 42 tofautitofauti ikiwemo American Black Achievement, American Music, Billboard Music, Brit, Grammy, MOBO, MTV Video Music, NAACP Image, Porin na nyingine kibao.
Kwa stori zote kali, Tu-follow
Facebook @Globalpublishers
Twitter @GlobalHabari
Instagram @GlobalPublishers
YouTube @GlobalTVTZ