Manchester, England
STAA wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic amemwambia mshambuliaji wa timu hiyo Anthony Martial, amsikilize kocha wake Jose Mourinho na kuachana na mawazo ya kuondoka Old Traff ord.
Martial ambaye alikuwa kwenye kiwango kizuri msimu uliopita msimu huu amekuwa akionyesha kiwango cha hali ya chini kitendo ambacho kimekuwa hakimvutii kocha wake Jose Mourinho. Kocha huyo amekuwa akimwambia kinda huyo raia wa Ufaransa kuwa anatakiwa kuongeza juhudi kama anataka kuendelea kuitumikia timu hiyo.

Hata hivyo, wakala wa mchezaji huyo Philippe Lamboley amenukuliwa mara kwa mara akisema kuwa anataka kumpeleka mchezaji huyo kwa mkopo kwa kuwa anaona hana nafasi Old Traff ord.
Zlatan amemwambia mchezaji huyo kama anataka kufanikiwa basi atulie na kumsikiliza kocha wake Jose Mourinho tu kwa sasa.
Kwa mujibu wa habari iliyoandikwa na gazeti la Telegraph, Zlatan amekuwa ndiye mshauri wa mara kwa mara wa kinda huyo na ushauri wake ndiyo umemzuia kuondoka na kujiunga na timu nyingine kwa mkopo.
Mbali na Zlatan, pia staa wa zamani wa Manchester United, Gary Neville amemwambia mchezaji huyo badala ya kuwaza kuondoka ajitahidi kuongeza juhudi uwanjani.