STORI: Na Wilbert Molandi | CHAMPIONI
DAR ES SALAAM: BEKI wa kati wa Yanga, Andrew Vicent ‘Dante’ anatarajiwa kuukosa mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Ngaya de Mbe ya Comoro huku Mtogo, Vincent Bossou akitarajiwa kutua leo Jumatano.
Dante anatarajiwa kuukosa mchezo huo kutokana na kuitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata kwenye mechi ya marudiano na TP Mazembe.
Yanga wanatarajiwa kuvaana na Wacomoro hao Jumapili hii mchezo utakaopigwa nchini
Comoro kabla ya kurudiana wiki mbili zijazo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema mchezaji ambaye atakaukosa mchezo huo ni Dante pekee, lakini wengine wapo fiti.
Saleh alisema, ni habari njema kwa mashabiki wa Yanga kuwa, wakati wakimkosa Dante, beki wao Bossou anatarajiwa kutua nchini leo Jumatano baada ya kumaliza majukumu yake ya timu ya taifa ya Togo iliyokuwa inashiriki Afcon 2017.
“Ni kweli kabisa hizo taarifa za Dante za kuikosa mechi na Ngaya de Mbe kutokana na
kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata mechi na Mazembe.
“Kadi hiyo, aliipata kwenye mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika tulipocheza na Mazembe nyumbani kwao baada ya Dante kumchezea vibaya Kalaba (Laurent).
“Lakini taarifa njema kwa mashabiki wa Yanga kuwa beki wao kipenzi Bossou, kesho (leo) anatarajiwa kutua nchini na moja kwa moja ataingia kambini kujiandaa na mchezo huo,” Saleh.
Kwa stori zote kali, Tu-follow
Facebook @Globalpublishers
Twitter @GlobalHabari
Instagram @GlobalPublishers
YouTube @GlobalTVTZ