Nionavyo Mimi ya Makonda ni Kama Hadithi ya Mwanakijiji
Imewekwa na on February 14th, 2017 , 09:24:15am

Nionavyo Mimi ya Makonda ni Kama Hadithi ya Mwanakijiji

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda

Na ELVAN STAMBULI| GAZETI LA UWAZI| NIONAVYO MIMI

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  ameanzisha vita dhidi ya madawa ya kulevya lakini staili yake ni kama hadithi ya mwanakijiji mmoja aliyepambana na chatu kuokoa watu waliokuwa wamemezwa na nyoka huyo. Hadithi hiyo inasema wanakijiji kadhaa walimezwa na chatu, ikatokea kijana mmoja akajitokeza na kusema ni lazima apambane na chatu huyo ili aokoe wale waliomezwa.

Alichukua kisu na kwenda kumpasua tumbo chatu bila tahadhari kwamba anaweza kuumiza walio tumboni, kwa bahati mbaya katika zoezi hilo alimkata kidole kijana mmoja aliyekuwa amemezwa, kijana yule baada ya kutoka tumboni mwa chatu alianza kulaumu kwa nini amemkata kidole na akadai fidia. Naamini katika hawa wanaotajwa na Makonda wapo watakaokuwa kama kijana yule mwanakijiji, wataumia na tayari wengine wanasema watamdai fidia Makonda.

Zoezi hili ni zuri lakini watuhumiwa wangechunguzwa kwanza kabla ya kutajwa. Nimefurahi kuona kuwa Makonda jana hakutaja majina 97 na badala yake kazi hiyo amempa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Nchini, Rogers Sianga.

Utaratibu huo utazuia waliokatwa kidole kulalamika. Ni kweli kwamba Tanzania imechafuka nje ya nchi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa vijana wetu wengi wamekamatwa wakijihusisha na biashara ya madawa ya kulevya katika nchi mbalimbali duniani, sasa ili kujisafisha lazima kupambana na wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

Ziliwahi kutolewa takwimu na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, aliposema kwamba zaidi ya vijana 400 wa Kitanzania wamekamatwa katika nchi mbalimbali duniani kwa kujihusisha na madawa ya kulevya.

Takwimu za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (ilikuwa ikiitwa hivyo 2014) zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2006 na Aprili, 2014, Watanzania 178 walikuwa wakitumikia vifungo mbalimbali nchini China pekee na wengine 113 wakiwa wamefungwa  nchini Brazil, wote wakiwa ni waliojihusisha na biashara hiyo ya madawa ya kulevya.

Mwaka 2014 taarifa za ukamataji kutoka Jeshi la Polisi, zilionyesha kuwa watuhumiwa 13,846 walikamatwa wakijihusisha na biashara ya madawa ya kulevya nchini kati ya Januari 2009 na Mei 2014.

Pamoja na watuhumiwa hao, taarifa inaonyesha pia kuwa, madawa yaliyokamatwa katika kipindi hicho ni pamoja na kilo 966.06 za heroin, kilo 363.7 za cocain, kilo 45,734 za mirungi na tani 212.071 za bangi, hii ilikuwa idadi kubwa sana.

Vikosikazi vya Kimataifa vya Kupambana na uhalifu katika Bahari ya Hindi, madawa ya kulevya na uharamia (Combined Task Force-150 (CMT-150), navyo vilifanikiwa kukamata shehena ya madawa ya kulevya aina ya heroin kilo 2,300, ikiwa ni katika kipindi cha Januari hadi Mei 2014 pekee. Dawa hizo zilikusudiwa kuingizwa katika  nchi za ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki, zikiwamo Tanzania, Kenya na Somalia.

Sifa ya Tanzania kimataifa imechafuka kutokana na vijana wengi kukamatwa wakijihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, hili hakuna anayepinga.

Baadhi ya wananchi, wakiungwa mkono na wataalamu wa masuala ya madawa na uhalifu wenye kuhusisha madawa ya kulevya wanaamini kuwa kukua kwa biashara hiyo nchini pamoja na vijana wengi kujihusisha nayo kunachangiwa zaidi na serikali kupata kigugumizi kuhusu wahusika wakuu wa biashara hiyo ambao wamebatizwa majina kama vigogo wa biashara za madawa ya kulevya au wazungu wa unga.

Inaelezwa kuwa, mtandao wa biashara ya madawa ya kulevya duniani, ukiwemo ule maarufu kwa jina la “Mafia,” huhakikisha wanawanasa viongozi katika kila ngazi ya uongozi au taasisi ya umma, lengo likiwa kuwatumia kufanikisha biashara yao haramu katika nchi husika.

Kutokana na biashara hiyo kufanyika katika mfumo wa mtandao wa kimataifa, wataalamu ndani ya vyombo vya dola vyenye kushughulikia tatizo hilo wanabainisha umuhimu wa kuikabili biashara hiyo kimtandao pia, katika ngazi ya kikanda kwa nchi jirani kushirikiana, pamoja na ngazi ya kimataifa. Majukwaa kama SADC, kupitia kamati ya yake ya usalama yakitumika itasaidia sana kukabiliana na kuenea kwa biashara hiyo katika nchi wanachama, hata hivyo, tunahitaji kusafisha nyumba yetu kwanza lakini tusafishe kwa kuzingatia sheria.

Madhara yanayoikabili nchi hivi sasa kutokana na vijana wengi kujitumbukiza kwenye biashara hiyo pamoja na utumiaji wa madawa hayo ni pamoja na kupungua kwa nguvu kazi, kuzorota kwa afya za watumiaji na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, madhara yote hayo yakiliathiri zaidi kundi la vijana ambao ni nguvukazi ya taifa.

Kutokana na athari za madawa hayo, taifa linaingia kwenye gharama zisizo za lazima, zikiwemo gharama za matibabu kwa vijana walioathirika. Takwimu zinaonyesha kuwa watumiaji 1,526, wakiwamo wanaume 1,321 na wanawake 205, wa madawa hayo, waliorodheshwa katika kipindi cha mwaka 2011 na Mei,2014, wanapatiwa  tiba ya dawa aina ya “methadone,” katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mwananyamala na Temeke, gharama inayotumika ingeweza kutumika katika shughuli zingine zenye tija. Watumiaji wa madawa ya kulevya wako katika mazingira hatarishi zaidi ya kupata maambukizi ya virusi vyenye kusababisha Ukimwi, kutokana na watumiaji hao kufanya ngono zembe pamoja  na kuchangia vifaa kama vile sindano wanazotumia kujidunga.

Magonjwa mengine yenye kusababishwa na madawa ya kulevya ni pamoja na homa ya ini, mapafu, moyo na kifua kikuu, yote yakiwa ni magonjwa hatari kwa maendeleo ya taifa. Uchambuzi zaidi kuhusu athari za matumizi ya madawa ya kulevya unaonyesha kuathiri kilimo cha mazao ya chakula na biashara, kutokana na wakulima katika mikoa mbalimbali nchini kubadili uelekeo kwa kujihusisha zaidi na kilimo cha bangi. Sheria itazame mianya yote yenye kutoa nafasi kuhamasisha matumizi ya madawa ya kulevya.

Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Madawa ya Kulevya nchini chini ya bosi mpya Kamishna Mkuu, Rogers Sianga inatakiwa ivalie njuga maeneo yanayotajwa kuathirika zaidi na madawa ya kulevya kama vile Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Arusha, Mwanza, Mbeya, Morogoro na Zanzibar, Nionavyo mimi; ni jukumu la jamii kusimamia kadhia hii ili itokomee kwa kufuata sheria na kamwe isiwe kupakana matope tu.

Tupia Comment Yako, Matusi Hapana

Stori zinazo husiana na ulizosoma