
Na Sweetbert Lukonge | CHAMPIONI
POINTI tatu ambazo Simba ilipokwa na Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji zimebaki hewani, kwani kuanzia maamuzi yalipotolewa wiki moja iliyopita, sasa ni zaidi ya siku saba Simba hawajapewa barua ya maamuzi hayo huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likidaiwa kuogopa kutoa barua hiyo.
Tangu Simba ipokwe pointi tatu na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ilizokuwa imepewa na Kamati ya Saa 72 kwa kosa la Kagera kudaiwa kumchezesha beki Mohammed Fakhi katika mchezo dhidi ya Mnyama akiwa na kadi tatu za njano, bado TFF imekaa na barua yake bila kuipeleka Simba.
Kila kukicha uongozi wa Simba umekuwa ukipiga kelele ukitaka upewe barua ya kupokwa pointi hizo lakini TFF imekuwa ikisuasua.
Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya TFF ambazo Championi Jumatatu limezipata, zimedai kuwa tangu Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji itoe maamuzi yake hayo, kuna mvutano mkubwa ambao umejitokeza ndani ya shirikisho hilo.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, wanadaiwa kumtisha Rais wa TFF, Jamal Malinzi, wakitaka kujiuzulu nafasi zao endapo tu Simba itapewa barua hiyo ya kupokwa pointi hizo tatu.
“Kutokana na hali hiyo ndiyo maana TFF imekuwa ikisuasua kuwapa Simba barua pamoja na ile ya kufungiwa kwa Haji Manara.
“Hata hivyo, ile ya Manara haiwaumizi kichwa sana kama hii ya pointi tatu, hiyo imekuja baada ya wajumbe hao kutoa msimamo wao,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema: “Hukumu zinaandaliwa na zitakapokuwa tayari watakabidhiwa barua, lakini hayo mambo mengine yanayosemwa ni propaganda tu.”
Hata hivyo, kwa hali ya kawaida, kitendo cha TFF kutowapa wahusika barua ya hukumu kwa zaidi ya siku saba sasa, kinaashiria kwamba kuna vitu vya chinichini vinavyoendelea ndani ya shirikisho hilo.