×

Simba Waishangaa Azam

Na Sweetbert Lukonge | CHAMPIONI | DAR ES SALAAM

JUZI Jumamosi timu ya Simba ilifanikiwa kutinga fainali ya michuano ya Kombe la FA baada ya kuichapa Azam FC bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kufuatia kipigo hicho, viongozi wa benchi la ufundi la Azam, walimshushia lawama mwamuzi wa mchezo huo, Mathew Akrama kutokana na kitendo chake cha kumwonyesha kadi nyekundu kiungo wa timu hiyo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Kutokana na hali hiyo, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amewashangaa Azam juu ya tuhuma zao hizo kwa mwamuzi huo na kudai kuwa Sure Boy alistahili kabisa kadi hiyo nyekundu, hivyo hawapaswi kumlaumu mwamuzi huyo.

“Jambo kubwa kama wanamichezo wanapaswa kukubaliana na mambo yote yaliojitokeza uwanjani kama mwamuzi alikuwa na upungufu, ulikuwa ni wa kawaida na wa kimchezo.

“Kama alimtoa mchezaji wao hata sisi alimwonyesha kadi nyekundu mchezaji wetu, Mohammed Ibrahim lakini tumekubaliana na hali hiyo,” alisema Mayanja na kuongeza:

“Katika mechi hiyo tulijipanga vilivyo kuhakikisha tunapata ushindi, tukijitahidi sana kuwajenga kisaikolojia wachezaji wetu lakini pia tuliwapatia majukumu ya kufanya uwanjani ili tuweze kuibuka na ushindi, nao wakafanya kama tulivyowaelekeza.”

Simba ina nafasi kubwa ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani. Mara ya mwisho Simba kushiriki michuano hiyo, ilikuwa ni mwaka 2013 baada ya kufanikiwa kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2011/12.

Leave a Comment