×

Rais Magufuli, Wahurumie, Hawa Wote Wanaume Zao Wameuawa Kwa Kupigwa Risasi

STORI: WAANDISHI WETU| UWAZI| HABARI

PWANI: Wanawake 22 ambao waume wao wameuawa na watu wasiojulikana katika Wilaya za Kibiti, Ikwiriri na Mkuranga mkoani Pwani wanaishi kwa hofu na shida kwani waliokuwa wakiwategemea roho zao zimekwenda baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

“Huku jamani sisi wajane, giza linapoingia wasiwasi na hofu tupu hutujaa. Tunakuwa hatujui nani atauawa. Hawa watu wameanza zamani kuua, tangu mwaka 2015, wajane tumekuwa hatuna wa kutusaidia,” alisema mjane mwingine.

STAILI YAO YA KUUA

Staili ya watoa roho hao ni kuua kwa risasi wakitumia bunduki aina ya SMG bila kuchukua pesa wala mali yoyote kutoka kwa marehemu huku wakiwa wamevaa kininja na wakitumia bodaboda hali inayotafsirika kuwa ni mauaji ya visasi.

KIJIJINI VIKINDU

Hofu nyingine kwa wajane hao ipo pia katika Kijiji cha Vikindu, Mkuranga kwani napo kuna kiongozi aliwahi kuuawa na wauaji hao Agosti 26, 2016. “Hofu ni kubwa hapa kijijini, hatuna raha na tunamuomba Rais Magufuli aliangalie hili na aone jinsi gani anaweza kutusaidia,” alisema mjane mmoja huku akiomba jina lake lisiandikwe. JARIBU MPAKANI Februari 22, 2017, katika Kijiki cha Jaribu Mpakani kulitokea mauaji ya watu watatu ambapo watu sita walivamia wakiwa na bunduki zinazosadikiwa kuwa ni aina ya Sub Machine Gun (SMG) waliwaua askari mmoja na raia wengine wawili, hivyo wajane watatu wamebaki na wanaishi kwa shida.

KUHUSU VIONGOZI WA VIJIJI

Kwa upande wa viongozi wa vijiji si rahisi kuamini lakini ndiyo ukweli ulivyo kwamba, idadi yao imefikia 22 wakiwa wameuawa kwa nyakati tofauti. Vijiji vilivyokosa viongozi wao ambao wamepigwa risasi na kuacha wajane ni pamoja na Kijiji cha Ikwiriri Kaskazini, Kijiji cha Mkuruwiti, Kijiji cha Muyui, Kijiji cha Makengeni, Kijiji cha Nyamunda, Jaribu Mpakani na Kibiti mjini.

VIJIJI VILIVYO NA WAJANE HAO

Vijiji vingine ambavyo wanaume wameuawa kwa risasi na kuacha wajane ni Ikwiriri wilayani Rufiji, Kitongoji cha Nyang’unda, Kijiji cha Nkwandala, Kijiji cha Bupu, Kitongoji cha Kazamoyo, Kijiji cha Kimanzichana, Kijiji cha Mkuruwili wilayani Mkuranga na Kijiji cha Nyang’hundu ambako wamebaki wajane. Kiongozi wa mwisho kuuawa ni Mwenyekiti wa CCM wa Njia Panda, Kijiji cha Muyuyu, Iddy Kirungi ambapo mwanaye, Nurdin Kirungi alijeruhiwa kwa risasi na wauaji hao Mei18, 2017.

Gazeti la Uwazi, mara kadhaa tangu mwaka 2015 limekuwa likiandika habari za watu waliopo kwenye baadhi ya misitu kwenye wilaya hizo kwamba, ndiyo wanaopanga mauaji ya kutisha ya polisi kwa lengo la kuchukua silaha kwa matumizi wanayoyajua wao, ikiwemo kuwaua viongozi wa vijiji wilayani humo.



UWAZI NA BARUA KWA MAGUFULI

Licha ya wajane hao kumuomba msaada kiongozi huyo wa nchi, Uwazi
liliwahi kumwandikia barua Rais Magufuli ikimweleza namna wananchi wa mkoa huo, hasa Mkuranga, Kibiti na Rufiji wanavyoishi kwa wasiwasi wakimwomba msaada wake kwa imani kwamba, anaweza kutuma jeshi maalum na kuwaangamiza wahalifu hao wanaoua kikatili viongozi wasio na hatia. Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo alipoulizwa kwa njia simu kuhusiana na hofu ya wajane hao, alikiri na kueleza kwamba matukio yaliyotokea siyo ya kawaida.

“Lazima uhofu, yaani upo nyumbani kwako unakula, mtu anakuja anakupiga risasi, watu wanasikia mlio, lazima wapate hofu, hilo ni jambo la kila mtu mwenye akili timamu, hata sisi viongozi halitupendezi jambo hili. Serikali inashughulikia wahalifu hao ili kuwaondolea hofu wananchi,” alisema mkuu huyo wa wilaya. Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, SACP Onesmo Lyanga amesema kazi yao ni kuhakikisha wahalifu wanapatikana. Juzi Jumapili Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba aliwatembelea wanachi wa Kibiti na kuwataka kuwafichua wahalifu hao.

Leave a Comment