
KATIKATI ya wiki iliyopita, Klabu ya Singida United ilikamilisha dili la kumsajili kipa wa Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’ kwa kumpa mkataba wa miaka miwili.
Barthez amejiunga na Singida baada ya kumaliza mkataba wake ndani ya Klabu ya Yanga huku akionekana hana tena nafasi ya kuendelea kuichezea timu hiyo chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na Mzambia, George Lwandamina.
Msimu ujao kipa huyo atakuwa akifundishwa na kocha wake wa zamani aliyekuwa naye Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.
Kipa huyo ambaye pia aliwahi kuichezea Simba, amefanya mahojiano maalum na Championi Jumatatu na kuzungumza mambo mengi na sababu hasa iliyomfanya ahamie Singida United inayodhaminiwa na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportPesa.
K W A N I N I U M E O N DOKA YANGA?
“Muda wa kuondoka ulifika ndiyo maana nikafanya hivyo.
“Najua Yanga ni timu kubwa na ilinipa kila kitu nilichokuwa nikihitaji, ukiangalia mataji ya Ligi Kuu Bara, Kombe la FA hata Ngao ya Jamii nimechukua nikiwa Yanga bila kusahau kushiriki michuano ya kimataifa, hivyo sikuwa na sababu ya kuendelea kung’ang’ania s e hemu moja wakati nimeshapata kila kitu.

NI NINI HASA KIMEKUFANYA UJIUNGE NA SINGIDA NA SIYO TIMU NYINGINE?
“Ni kutokana na maamuzi yangu si kitu kingine, unajua kila mtu huwa na maamuzi yake, kwa hiyo binafsi niliona huu ni muda sahihi wa mimi kuja huku kwa sababu wao wenyewe walionyesha nia ya kunihitaji zaidi.
“Lakini pia ukiangalia hii timu imejipanga kweli kuleta changamoto mpya katika ligi yetu, nikiwa kama mchezaji huwa napenda kucheza timu yenye kuleta ushindani.
“Na jambo kubwa ambalo ninalotaka kulifanya hapa ni kuipa timu mafanikio kama yale niliyoyapata nikiwa Yanga.
U N A J I S I K I A J E KUFUNDISHWA TENA NA PLUIJM?
“Ni vizuri tu kwa sababu tangu nianze kufanya naye kazi nimeona ni kocha mzuri ambaye anapenda timu yake ifanikiwe muda wote. Kutokana na hilo naamini huku pia tutafanikiwa chini yake.
WEWE NA NIZAR KHALFAN NDIYO WAKONGWE HAPA, UNAWAAMBIA NINI VIJANA WALIOSALIA?
“Tushirikiane tu kuijenga timu na naamini ukongwe wetu tutautumia vizuri kuwapa hamasa hawa wenzetu ili tu timu ifanye vizuri.
UNA LIPI LA KUWAAMBIA MASHABIKI WA SINGIDA UNITED
“Wanachotakiwa ni kuendelea kuisapoti timu yao wakati wote ili tuweze kufikia malengo ambayo yapo kwani hapa kila mmoja anahitaji nguvu ya mwenzake kufanikisha jambo.
NENO LOLOTE KWA SOKA LA BONGO
“Nadhani kila siku kuna mabadiliko, nauona msimu ujao ukiwa na ushindani mkubwa kutokana na timu kujipanga vizuri.
“Ukiangalia zamani Simba, Yanga na Azam ndizo zilizokuwa zinaonekana kuwa vizuri pekee, lakini naamini msimu ujao Singida nayo itakuwa katika kundi hilo.
“Nasema hivyo kutokana na kwamba huu udhamini ulioletwa na SportsPesa umechangia timu kujengeka vizuri,” anasema Barthez.