×

Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Ndoto Zitimie

GEORGE Majaba, ambaye kabla ya Septemba 27, mwaka huu hakuwahi kuwa na ndoto za kumiliki nyumba katika ardhi ya Jiji la Dar es Salaam, hatimaye amebakiza saa 48 tu kabla hajawa mmoja kati ya wamiliki wachache wa nyumba za kisasa nchini.

Tukio la kukabidhiwa nyumba yake hiyo, yenye vyumba vitatu vya kulala, ikiwemo Master Bed Room, sebule, jiko, choo, bafu na chumba cha kulia chakula, ambayo pia imeunganishwa kabisa na nishati ya umeme litafanyika Jumanne ijayo mara tu baada ya yeye kuwasili akitokea Dodoma, ambako ndipo yalipo makazi yake kwa sasa.

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho ambao ndiyo waendeshaji wa bahati nasibu hiyo, Majaba, ambaye ni kondakta wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kati ya Dodoma Mjini na Vijijini, anatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam Jumanne.

Baada ya kuwasili Ubungo Terminal, Majaba atakwenda katika ofisi za Global Group, zilizopo Sinza Mori zinazotazamana na Wanyama Hotel, ambako atasalimiana na wafanyakazi wa Global Publishers na kufanya mahojiano mafupi, kabla ya kupelekwa Bunju B, ilipo nyumba hiyo kwa ajili ya zoezi la kukabidhiwa.

“Tunataka kufanya kitu kidogo tofauti na cha kumtia faraja mshindi wetu, kwa maana hiyo tumeandaa mapokezi maalum, tumeandaa pikipiki na magari ambayo yatampokea Ubungo Terminal na kuja naye hadi ofisini kwetu (maeneo ya Sinza Mori, zamani Johanesburg Hotel).

“Pale kutakuwa na utambulisho rasmi wa mshindi wetu ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano na vyombo vya habari kisha tutaanza safari ya kuelekea nyumbani kwake kwa ajili ya kumkabidhi nyumba yake,” alisema.

“Tumeamua kumpa nyumba ikiwa kamili kabisa, atakachofanya yeye ni kuja na begi lake na kuanza maisha, hiyo yote ni kuonyesha jinsi gani Global Publishers imedhamiria kubadili maisha ya wasomaji wake, pamoja na thamani kubwa ya nyumba, lakini tumeona tumuongezee na nishati hii muhimu ili kumpunguzia jukumu la kuhangaika kuingiza umeme,” alisema Mrisho.

Hii ni mara ya pili kwa Global Publishers, kampuni pekee ya uchapaji magazeti katika historia, kuwahi kutoa zawadi ya nyumba kwa wasomaji wake.

Kabla ya kupatikana kwa mshindi wa awamu hii ya pili, bahati nasibu hiyo ilifanya droo ndogo tano katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, ambako wasomaji zaidi ya 30 walijipatia zawadi kemkem, zikiwemo pikipiki, ving’amuzi, televisheni flat screen, simu za kisasa za mikononi, kofia na fulana.

Katika Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Kwanza, mshindi wake alikuwa ni Nelly Mwangosi, mjasiriamali mwenyeji wa Iringa, ambaye nyumba yake ipo Salasala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

SHUHUDIA LIVE: Birthday ya Aunty Ezekiel, Masaki Dar ni Kufuru

Leave a Comment