
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema matokeo ya awali waliyoyapokea kutoka vituo vya kupigia kura yanaonyesha kuwa, mpaka sasa CCM inaongoza katika Kata 42 kati ya 43 zilizoshiriki uchaguzi mdogo uliofanyika jana maeneo mbalimbali hapa nchini.

Polepole ameyasema hayo leo Jumatatu, Novemba 22, 2017 alipokuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.
“CCM imeshinda kwa zaidi ya asilimia 90, hivyo ushindi huo unatokana na jinsi chama chetu kilivyokuwa kimejipanga vilivyo tofauti na miaka ya nyuma. Chama kilijidhatiti na kila mgombea wetu alikuwa na kazi moja tu ya kuinadi Ilani ya CCM. Hivyo ilikuwa rahisi sana kwetu kushinda,” amesema Polepole.
Katibu huyo amesema kuwa licha ya maeneo mbalimbali ambayo ulifanyika uchaguzi huo umefanyika vizuri, lakini baadhi ya maeneo kuna changamoto mbalimbali ikiwemo watu kupigwa na kutekwa.