IKIWA ni siku chache tangu kupata ajali kwa Baunsa wa Msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, Mwarabu Fighter ambaye tayari amesharuhusiwa kurudi nyumbani akitokea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu, mke wa Baunsa huyo, Mama Tarick amesema lakini hali ya mumewe bado siyo nzuri sana lakini wanamshukuru Mungu kwa jinsi alipofikia anaendelea vizuri.
Akipiga stori na Global TV Online, Mama Tarick amesema kuwa siku ya tukio aliagana na mumewe majira ya saa 11 alfajiri akielekea kwenye shughuli zake za kila siku, lakini dakika chache baadaye alimpigia simu na kumweleza kuwa amepata ajali na hajui endapo atapona.
“Aliponiambia vile na simu ikakata, nilikurupuka kitandani nikatoka mbio mbio, nilipofika getini nikakuta chupa niliipiga teke ikanikata, damu nyingi zilivuja lakini sikujali, nilienda hivyo hivyo hadi Hospitali ya Lugalo ambapo alipatiwa matibabu ya awali, baadaye tulipandishwa kwenye ambulance na kupelekwa Muhimbili. Mpaka sasa nina jeraha kubwa la kukatwa chupa, lakini nachechema nalo hivyo hivyo,” amesema Mama Tarick.
Aidha, mama huyo amewashukuru madakrati kwa kuokoa uhai wa mumewe na kuelza kuwa kipimo cha CT Scan kilionyesha ana uvimbe kidogo kichwani ambapo akipewa dawa utapona taratibu, pia amefunguka kwamba wameelekezwa na madaktari kwamba, mgonjwa huyo apewe muda mwingi wa kupumzika na hatakiwi ashike simu mara kwa mara.