
YANGA ina mpango wa kumleta msaidizi wa kipa wao Youthe Rostand ambapo habari mbaya ni kuwa kipa ambaye walipanga kumsajili Mohammed Abdulrahman Wawesha wa JKU, ameikacha timu hiyo na kujiunga na JKT Tanzania ambayo ataichezea kwa msimu ujao.
Kikosi hicho cha Yanga kinaendelea na mpango wa kumleta mbadala wa kipa huyo raia wa Cameroon, ambapo Wawesha na kipa wa TP Mazembe ya Congo, Ley Matampi majina yao ndiyo yalikuwa kwenye meza ya usajili ya mabosi wa timu hiyo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Katibu Mkuu wa JKU, Sadu Ujudi Maalim amesema kuwa tayari wao na JKT Tanzania wameshamalizana na kipa huyo ambaye ni tegemeo katika timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ atajiunga na timu hiyo mara baada ya kumalizika kwa Kombe la Kagame ambalo litaanza Ijumaa hii.
“Kama Yanga walikuwa wanamtaka kipa wetu Mohammed Abdulrahman basi hiyo itakuwa kwao maana tayari sisi tumeshamalizana na JKT Tanzania kwa kila kitu juu ya usajili wake huko na kilichokua kinakwamisha ni usajili kutofunguliwa kwa wakati (usajili ulifunguliwa Julai 15).
“Kilichobaki kwa sasa ni yeye tu kwenda huko na kupeleka barua yake maana kila kitu tayari kimeshakamilika, baada ya michuano hii ya Kagame basi ataenda kujiunga na timu yake mpya,” alisema Ujudi.
Stori: Said Ally, Dar es Salaam
