TUKIO la kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere kisiwani Ukara Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, limeathiri kada mbalimbali za Watanzania ambapo pia limegusa kwenye sekta ya michezo kutokana na timu ya Stand United baadhi ya wachezaji wake kuwapoteza wapendwa wao kwenye ajali hiyo.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Alhamisi iliyopita ambapo watu 224 walipoteza maisha mara baada ya kivuko hicho kuzama kisiwani humo.
Timu za ligi kuu ambazo zinatoka Kanda ya Ziwa ambako kumetokea tukio hilo ni pamoja na Stand United na Mwadui FC (Shinyanga), Biashara United (Mara) na Mbao FC (Mwanza).
Kocha Msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal ‘Bilo’ ameliambia Championi Jumatatu, kuwa tukio hilo limewagusa wao kutokana na wachezaji wao wakiwemo Sixtus Sabilo na Erick Mulilo kuwapoteza watu wao wa karibu kwenye ajali hiyo. “Kwetu ajali hiyo ya kuzama kwa MV Nyerere imetugusa kwa namna moja au nyingine kwa sababu kuna wachezaji wetu wanne ambao wamewapoteza wapendwa wao.
“Kuna wachezaji ambao wanatokea Ukerewe hapohapo kabisa ambapo tukio hilo limetokea. Kuna Sixtus Sabilo, Erick Mulilo na Makenzi Kapinga na Datius Peter,” alisema Bilo.
Championi Jumatatu, lilimtafuta Sabilo ambapo alipopatikana alisema: “Nashukuru Mungu hadi dakika hii sijajulishwa kwamba kuna ndugu yangu wa karibu alikuwemo mule ila kuna marafiki zangu wengi sana wamepoteza maisha na jamaa zangu wa karibu ila siyo ndugu kabisa.
“Ni marafiki zangu tu wa karibu ndiyo walikuwemo lakini siyo ndugu zangu, nimefuatilia kwa karibu sana, hakuna ndugu zangu waliokuwepo kwenye huo usafiri, lakini ni marafiki zangu wa karibu ndio waliopoteza maisha.”
Championi pia liliwatafuta, Mwenyekiti wa Biashara United, Selaman Mataso na Katibu wa Mwadui FC, Ramadhan Kilao ambao kwao walisema mambo ni shwari.
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
WAZIRI MKUU AONGOZA MAZISHI KITAIFA UKARA – VIDEO