×

MTUHUMIWA KUTEKA, KUUA MTOTO HUYU HAPA!

MBEYA: SIKU chache baada ya kukamatwa kwa kijana Mussa Mbelechamo (27) anayetuhumiwa kumteka kisha kumuua mtoto Junior Bakari Siame (8), mwanafunzi wa darasa la tatu wa Shule ya Msingi Hayanga jijini Mbeya na kutimkia mkoani Iringa, hatimaye amerejeshwa Kituo Kikuu cha Polisi jijini hapa na picha yake kunaswa na wanahabari.

 

Mtuhumiwa huyo alikamatwa Aprili 13, mwaka huu, Ipogolo mjini Iringa baada ya kudaiwa kutenda kosa hilo Aprili 9, mwaka huu eneo la Mlima Nyoka, nje kidogo ya Jiji la Mbeya.

Mara baada ya kukamatwa, baadhi ya wakazi waliomshuhudia kijana huyo walionekana kushangazwa na simulizi yake hasa baada ya kumuona akiwa na umri mdogo.

 

“Mh! Yaani huyu kweli ndio alipata ujasiri wa kumteka mtoto, kwenda naye hadi nyumbani kwao kubadili nguo kisha kutoka naye? Kila mtu na moyo wake, hafananii kabisa na ukatili huu,” alisikika mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwakipesile kituoni hapo.

Hata hivyo, mtuhumiwa huyo baada ya kukamatwa na kuhojiwa na Polisi, anadaiwa kukiri kutenda tukio hilo ambapo kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Ulrich Matei, mtuhumiwa huyo alisema lengo la kumteka ilikuwa ni kumshinikiza mzazi wa mtoto amlipe hongo ya Tsh 10 milioni ili amwachie.

 

Alisema alimchukua mtoto na kwenda naye nyumbani kwao akabadilisha nguo za shule na kuvaa ‘truck suit’ ambapo alichukua pia namba ya simu ya fundi wa friji jirani na alipokuwa anaishi mtoto huyo iliyoandikwa kwenye bango la fundi.

Aliendelea kueleza kuwa, alimchukua mtoto na kwenda naye hadi kituo cha mabasi cha Nane Nane na baadaye walipanda daladala kuelekea Nsalaga ambapo alimnunulia juisi kisha wakaanza kutembea kwa miguu hadi Mlima Nyoka kwenye shamba la mahindi ambapo mtoto alianza kupiga kelele; ndipo Mussa alipomziba mdomo na pua na kumfanya akose hewa na kuanguka chini na muda mfupi baaaye alipoteza maisha.

 

Alidai kuwa, baada ya kupoteza maisha alichukua nguo ya marehemu kisha kumfunga shingoni aonekane amenyongwa ndipo aliondoka hadi Uyole kisha kupanda gari hadi Makambako alipolala; asubuhi alielekea Iringa.

Alipofika Iringa aliomba kuletewa begi kutoka Mbeya na rafiki yake wakati huo aliomba kutumiwa pesa ambapo Polisi waliweka mtego na kumtumia shilingi laki moja hata hivyo pesa hiyo hakufanikiwa kuitoa.

 

Juhudi za Polisi zilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa na kumrejesha Mbeya ambako Mussa aliwaonyesha mwili wa mtoto ulipo na Polisi waliuchukua mwili wa marehemu hadi Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa ajili ya uchunguzi na baadaye ukazikwa.

Aidha, kamanda huyo alitoa wito kwa wazazi, walimu na walezi kutoa elimu kwa watoto ili waweze kutembea wengi na pia watoto wasikubali kuitwa na watu wasiowafahamu.

 

Kamanda Matei alisema kitendo kilichofanywa na mtuhumiwa ni cha kinyama na ameagiza wakuu wa Polisi wilaya zote kutoa elimu kwa wananchi ili kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Hata hivyo, Matei alisema ni vema watu wanaotoka kifungoni ikabidhiwe jamii kwa ufuatiliaji zaidi wa mwenendo wao kwani uchunguzi wa Polisi umebaini mtuhumiwa kuachiwa Februari, mwaka huu alipokuwa akitumikia kifungo cha miaka thelathini kwa tuhuma ambazo hazikujulikana.