
UONGOZI wa Klabu ya Nkana ya nchini Zambia, umeweka wazi kuwa hawajavunja mkataba na beki wao, Mtanzania, Hassan Kessy kama inavyoelezwa kuwa ameachana na timu hiyo.
Juzi mchana kuliiibuka taarifa za beki huyo kuwa ameachwa na timu hiyo kwa kuwa hakuwepo katika mchezo wa ligi kuu ya nchi hiyo dhidi ya Power Dynamo uliopigwa kwenye Uwanja Arthur Davies uliopo Kitwe nchini humo huku Nkana ikipoteza kwa kipigo cha mabao 3-0.
Championi lilimtafuta Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Charles Chakatazya, alisema kuwa Nkana haijavunja mkataba na beki huyo kama inavyoelezwa kwani hakuwepo kwa muda kutokana na matatizo ya kifamilia.

“Kessy wala hatujavunja naye mkataba kama inavyoelezwa na siyo kweli bado ni mchezaji wetu kutokana na mkataba uliopo.
“Lakini hakuwepo kwa sababu ya matatizo ya kifamilia, alienda Tanzania kumuuguza baba yake mzazi anayeishi Morogoro ambaye alikuwa mgonjwa ila tunavyoongea ameshafika Kitwe kuungana na timu, hatujavunja mkataba wala yeye hakutaka kuvunja mkataba, bado tuna mipango naye mirefu,” alisema Chakatazya.