×

‘Mwambieni Ole Huu Siyo Muda wa Kuchekacheka’

STRAIKA wa zamani Robin van Persie amemshauri kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer kuwa na uso wa kazi bada ya kushuhudia timu yake ikichapwa mabao 2-0 kutoka kwa Arsenal, lakini kocha huyo akawa anaonyesha tabasamu. Van Persie, straika wa zamani wa Arsenal na

 

Manchester United aliyasema hayo akiwa mchambuzi wa soka kwenye runinga baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa Premier League. Kupitia runinga, Solskjaer alionyesha uso wa tabasamu na kucheka kidogo wakati alipokuwa akihojiwa baada ya mchezo huo.

“Nimemtazama Ole bado anaonyesha yeye anataka kuwa mtu mzuri, binafsi ningependa kumuona akiwa na uso wa kazi, yaani amaanishe anachokizungumza kutokana na matokeo.

Anatabasamu na kucheka baada ya mchezo, huu siyo muda wa yeye kutabasamutabasamu,” alisema Van Persie. Alipoulizwa kama matokeo hayo yanaweza kuhatarisha uaminifu wa kocha kwa wachezaji, Van Persie alisema yanaweza kuwa na athari.

 

“Unapokuwa kocha unahitaji kuogopwa kiasi, lakini muhimu unatakiwa kuwa na mipango sahihi, ukikosa njia sahihi za kupita kwa wapinzani wako wanakuadhibu  na unatakiwa kuwa mkali kwa wachezaji, kama hafanyi kile unachomuelekeza mechi inayofuata unamwambia hatacheza,” alisema.

 

Ushindi kwa United ungeweza kuisogeza timu kuingia nafasi ya nne kwa kuwa Chelsea inayoshika nafasi ya nne ilipata sare dhidi ya Brighton, wakati Tottenham na Wolves wanaowafukuzia wote wakipoteza mechi zao.

Leave a Comment