IMEZOELEKA kila mara inapokaribia mechi ya Simba dhidi ya Yanga, timu hizo zimekuwa na kawaida ya kusafiri kwenda kujificha lakini Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amefichua kuwa safari hii wameshindwa kufanya hivyo kutokana na kila kitu ambacho walikuwa wanakitaka kuwepo ikiwemo Uwanja wa Simba Mo Arena wanaoumiliki.
Kesho Jumamosi, Simba watakuwa wenyeji wa Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara msimu huu ambayo itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Senzo ameliambia Championi Ijumaa, kuwa walishindwa kusafiri kwenda sehemu yoyote kwa ajili ya mechi hiyo na kubakia Dar kutokana na vitu vyote ambavyo walikuwa wanavihitaji kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo kuwepo Dar ukiwemo uwanja wao wanaoumiliki kule Bunju.

“Huko nyuma timu ilikuwa inasafiri na kwenda sehemu nyingine kwa sababu ya kutafuta mahali ambapo tutafanya mazoezi kuelekea mechi hii lakini kwa msimu huu mambo yamekuwa tofauti.” alimaliza Senzo.