
UNAWEZA kusema hivi sasa ubingwa wa Ligi Kuu Bara hauna mwenyewe licha ya kwamba Simba ndiyo inaongoza ligi ikiwaacha wapinzani wao wa jadi, Yanga kwa pointi kumi.
Simba ikiwa imecheza mechi 14, imekusanya pointi 35, Yanga katika mechi 12, imekusanya pointi 25. Kutokana na gepu hilo, Simba walianza kujiaminisha mapema kwamba watakuwa mabingwa.
Lakini ile sare ya 2-2 waliyoipata dhidi ya Yanga Jumamosi iliyopita imewashtua wengi na kuanza kuamini kwamba, Yanga pia inaweza kuwa bingwa, hivyo ishu hiyo ipo mikononi mwao kuamua wawe mabingwa au wawaachie Simba.

Wanayanga hivi sasa wanatamba kwamba ile shughuli waliyowaonyesha Simba Uwanja wa Taifa juzikati ni ya kitoto, mziki kamili wataupata wakikutana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.
Yanga ambao ni mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara wakichukua ubingwa huo mara 27, katika dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Desemba 15, mwaka jana, limeongeza makali ya kikosi chao ambacho kwa sasa kina wachezaji wapya watano ambao moja kwa moja wamepata nafasi kwenye kikosi cha kwanza kinachonolewa na Charles Boniface Mkwasa.
Kwa namna mambo yalivyo kwa sasa ndani ya Yanga, Mkwasa ambaye ni kaimu kocha mkuu wa kikosi hicho, hana mashaka yoyote ya kufanya vizuri hata akitakiwa kucheza kwa siku mbili mfululizo.
Ipo hivi; nyota hao wapya ambao ni Haruna Niyonzima, Ditram Nchimbi, Yikpe Gnamien, Adeyum Saleh na Tariq Seif, wamefanya Yanga kuwa na kikosi kipana kinachoweza kutengeneza vikosi viwili vya nguvu.
Vikosi hivyo kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi ikaamua kuipangia Yanga mechi moja Dar na nyingine mkoani, basi Wanayanga watakuwa na jukumu la kugawana kwenda kushangilia, kisha kurudi na pointi zote.
Leo Alhamisi, Yanga inatarajiwa kucheza na Mtibwa Sugar katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amaan uliopo Unguja, Zanzibar. Kesho Ijumaa uwanjani hapo, Simba nayo itacheza dhidi ya Azam. Washindi wa mechi hizo watacheza fainali Jumatatu ijayo ya Januari 13.
Mashabiki wa Yanga baada ya kubaini kwamba wana vikosi viwili vya nguvu, wanawauliza Simba wawapangie kikosi gani kama wakikutana kwenye fainali ya Mapinduzi kwa sababu kwenye ligi tu waliwatoa jasho wakati wakiwa bado hawajakaa sawa.
Ukiangali vikosi viwili vya Yanga vinaweza kuwa hivi; Cha kwanza kitaundwa na Farouk Shikalo, Juma Abdul, Adeyum Saleh, Lamine Moro, Kelvin Yondani, Abdulaziz Makame, Papy Thishimbi, Haruna Niyonzima, Ditram Nchimbi, Tariq Seif na Patrick Sibomana.
Kikosi cha pili; Metacha Mnata, Paul Godfrey, Ally Sonso, Adrew Vicent ‘Dante’, Ally Ally, Deus Kaseka, Mrisho Ngasa, Mohamed Issa ‘Mo Banka’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Yikpe Gnamien na Mapinduzi Balama.
Wachezaji wengine waliobaki ambao ni Ramadhan Kabwili, Japhary Mohamed, Cleophace Peter, Said Makapu, Gustapha Suleiman, Mustapha Suleiman, watakuwa wapo benchi kuangalia namna ya kuchukua nafasi.
Mkwasa ameliambia Spoti Xtra kuwa, usajili ambao wanaufanya kwenye dirisha dogo ni maalumu kwa ajili ya maboresho ya kikosi chao na wana imani watafanya vema kwenye michuano yote watakayocheza ikiwemo Ligi Kuu Bara.
“Sina mashaka na Niyonzima yeye ni mkomavu, hana matatizo, Nchimbi ameanza kucheza tayari hata Tariq ameonesha uwezo wake, hivyo hawa wote wakicheza mechi nyingine mbili watakuwa wameonyesha ukomavu wa hali ya juu, timu itakaa sawa zaidi.
“Kila mchezaji nina imani naye na matumaini yangu watafanya vizuri, nimesikia mashabiki wanalalamika kuwa Yikpe ni mzito na Adeyum mzembe, mechi za kwanza kwao lazima ziwasumbue kwani bado hawajazoeana, ila wakicheza mechi nyingi zinatosha kuwaimarisha zaidi,” alisema Mkwasa.
STORI NA LUNYAMADZO MLYUKA