
NAHODHA wa Azam FC, Aggrey Morris, amefiwa na mkewe usiku wa leo jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kumalizika mchezo wa nusu fainali ya Mapinduzi Cup dhidi ya Simba. Aggrey hakuwepo kwenye kikosi cha Azam kilichoenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya kumuuguza mkewe ambaye alikuwa mjamzito.
Timu ya Azam, kupitia ukurasa wa Instagram, imesema:
Azam FC tumepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mke wa nahodha wetu, Aggrey Moris, aliyefariki dunia jana jioni wakati akiwa kwenye harakati za kujifungua.
Tunatoa salamu zetu za pole kwenda kwa familia ya Morris, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki na wote walioguswa na msiba huo.
Azam FC tunaungana na familia ya marehemu na tunamuomba Mwenyezi Mungu, awajalie nguvu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Bwana ametoa na Bwana Ametwaa, Jina lake lihimidiwe. Amen.
