
Polisi wanawake mkoa wa Mwanza wamedhamiria kukomesha na kutokomeza vitendo vya ukatili pamoja na wanawake wanofanya biashara haramu ya ngono katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Safia Jongo amesema askari wa kike wana nafasi kubwa ya kutokomeza ukatili kwa kutoa elimu kwa jamii pamoja na wadada wanaofanya biashara ya kuuza miili yao ili kukomesha vitendo hivyo kwani kwa sasa kuna maradhi mengi yanayosababishwa na kufanya ngono kiholela.
“Wanawake wangapi wanafanya biashara ya kujiuza huko mtaani? Je, tuna uhakika waume zetu wamesalimika kweli? Sisi kama polisi wanawake tutawakamata hawa machangudoa. Tunayo madawati maalum ambapo tutawapa elimu waachane na biashara hiyo wafanye biashara nyingine halali.
“Si tu wanawake wanaofanyiwa ukatili, lakini pia wapo wanaume wengi wanaofanyiwa ukatili na baadhi yao wamekuwa wakiripoti na sisi tunachukua hatua, lakini tatizo la wanaume wamekuwa aoga kusema kama wanafanyiwa ukatili. Tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha tunakomesha ukatili huo kwa wanawake, watoto na wanaume.”