WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Technolojia, Profesa Joyce Ndalichako na Balozi wa China nchini, Mhe Wang Kel, jana Januari 18, 2020, wameshiriki uwekaji wa jiwe la msingi la sekondari ya mfano ya masomo ya sayansi mkoani Arusha iliyopewa jina la mkuu wa mkoa huo Mrisho Gambo.
Shule hiyo ya kisasa ambayo kwa mkoa wa Arusha ni ya kwanza itakayokuwa ikiendeshwa kwa mfumo wa kisayansi (STEM)yaani Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati, ipo katika kata ya Olasiti jijini ambayo hadi sasa tayari madarasa manane ya kisasa yamekamilika na tayari wanafunzi wamenza kuyatumia.
Pia ina maabara nne za kisasa, chumba cha kompyuta, nyumba za walimu na madawati ambapo madarasa mengine na jengo la utawala bado vikiendelea kujengwa.

Akizungumza baada ya kutembelea na kukagua shule hiyo, Ndalichako amepongeza jitihada za uongozi wa mkoa wa Arusha kwa mikakati yake ya kuboresha elimu mkoani humo na nchi nzima ambapo amesema kama serikali wanataka shule hiyo kuwa ya mfano hapa nchini kwa kuwa itakuwa na uwezo wa kuchukuwa wanafunzi wa sayansi kwa kiasi kikubwa hivyo kusaidia kupata wataalam wa kutosha katika sayansi na technolojia.

Naye Gambo ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wote walioshiriki kufanikisha ujenzi wa shule hiyo kwa namna moja ama nyingine na kusema kuwa kama mkoa wameamua kuwekeza katika elimu kutokana na kutambua umuhimu wa elimu huku akiwatoa hofu wale wote wanaodhani amekuwa akifanya maendeleo hayo kwa nia ya kutaka ubunge wa jiji la Arusha.
Ili kufanikisha ujenzi wa shule hiyo wadau mbalimbali wamechangia katika nyanja mbalimbali ambapo Benki ya I & M imechangia madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni kumi.
Akizungumza katika hafla hiyo Afisa mtendaji Mkuu wa Benki ya I&M, Baseer Mohammed, amesema benki hiyo imekuwa ikitoa sehemu ya faida yake kusaidia jamii.

“Mheshimiwa waziri I & M Bank leo imetoa madawati haya 100 kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za kutoa elimu bure ili watoto wengi waweze kunufaika na elimu bure,” alisema Baseer.
Mbali na wadau hao ukiwemo ubalozi wa China, CRDB Bank imejenga darasa moja katika shule hiyo lenye thamani ya Shilingi milioni 20.

Meneja wa CRDB Bank Kanda ya Kaskazini, Chiku Issa, alisema benki hiyo imekuwa na desturi ya kusaidia jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya,na nyinginezo.
“Leo CRDB Bank imekabidhi darasa lenye thamani ya Shilingi milioni ishirini ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kutoa elimu bure,” alisema Chiku.