
MBUNGE wa jimbo la Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, wamejitetea kutofutiwa dhamana yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kudai kuwa walilazimika kusafiri kwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ya Mdee.
Katika shauri hilo namba 112 la mwaka 2018 Bulaya na Mdee wanashtakiwa na vingozi saba akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), Freman Mbowe ambapo wawili hao walisafiri nje ya nchi bila ruhusa ya mahakama, kwa mujibu wa masharti ya dhamana yao.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa katibu mkuu, Dkt. Vincent Mashinji, Mbunge Tarime John Heche, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Vijijini Esther Matiko, Mbunge wa Jimbo la Kibamba ambaye hivi sasa ni Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, na katibu Mkuu upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu.
Akijitetea, Halima Mdee amedai kuwa mnamo Januari 6 mwaka huu, daktari wake wa hospitali ya Aga Khan liyemtaja kwa jina la Kaguta, aliiandikia barua mahakama hiyo kwamba mgonjwa wake ambaye ni mtuhumiwa mwenye kesi, Halima Mdee, alitakiwa akapate matibabu ya ziada ambayo hospitali za ndani ya nchi wzimeshindwa kuzitoa.
Mdee amedai kuwa taarifa ya kwenda kwenye matibabu aliitoa mara mbili mahakamani hapo, Novemba 25 na Desemba 18 mbele ya Wakili wa serikali, Sylvia Mitanto, na wakili wa upande wa utetezi na pia alimuomba hakimu maombi binafsi ya kusafiri kwake.
Kwa upande wake, Esther Bulaya amedai kuwa alipewa jukumu la kumuangalia Mdee akiwa kwenye matibabu huko nje ya nchi kwa kuwa yeye ni mwanamke mwenzake na mama wa Halima ni mzee sana.
Akipinga hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamiz, Wankyo Simon, amedai kuwa sababu zilizotolewa hazina msingi na zinatosha kuifanya mahakama hiyo kufuta dhamana zao kwa kukiuka sharti la msingi la kusafiri nje ya nchi bila kibali.
Wankyo ameongezea kuwa masharti ya dhamana yaliwataka kupata kibali kutoka mahakamani na si kuwasilisha taarifa ili waweze kusafiri nje ya nchi. Naye wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi, amedai kuwa ni mara ya pili washtakiwa wanakiuka masharti ya dhamana hivyo akaiomba mahakama kufuta dhamana zao au kushikilia hati zao za kusafiria kama mbadala.
Wakili wa utetezi, John Mallya, akitetea hoja hizo amedai kuwa watuhumiwa hawakukamatwa bali walikuja mahakamani wenyewe, hawakupita kwenye mipaka ya nchi kwa njia za panya na hawana mpango wa kukimbia nchi hivyo hakuna sababu ya kufuta dhamana zao.
Naye wakili wa utetezi, Hekima Mwasipu, amedai kuwa barua kuandikwa na mshtakiwa si takwa la kisheria bali la msingi ilikuwa mahakama kupata taarifa.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Simba amesema atatoa uamuzi juu ya kufutwa au kutofutwa kwa dhamana hizo Januari 31 mwaka huu na kesi ya msingi itaendelea kusikilizwa kesho Januari 22, mwaka huu.