BAADA ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kususia mkono wa Spika wa Bunge la Wawakilishi nchini Marekani, Nancy Pelosi, spika huyo naye amemjibu kwa kuichana hotuba yake (Trump), mambo ambayo ni baadhi tu ya vitimbi vilivyodhihirisha mgawanyiko mkali wa kisiasa nchini Marekani.
Hilo lilitokea wakati Trump alipotoa hotuba kuhusu hali ya uchumi wa nchi hiyo.
Tofauti na ilivyozoeleka kuwa hotuba ya rais wa Marekani kuhusu hali ya nchi ni muda wa maridhiano kisiasa, mazingira katika kikao cha Congress kilichowaleta pamoja wajumbe wa baraza la wawakilishi na maseneta yaliakisi mpasuko mkali wa kisiasa muda wote wa saa moja na dakika 18 wa hotuba ya Trump.
Zoezi zima lilianza vibaya pale Rais Trump alipokataa kuupokea mkono alionyooshewa na spika wa baraza la wawakilishi, Bi Nancy Pelosi, na kuuacha ukining’inia hewani. Na lilimalizika kwa hatua ya Pelosi kumjibu Trump kwa mtindo wa jino kwa jino, alipoichana vipande-vipande nakala ya hotuba ya Trump aliyokuwa amekabidhiwa, mara tu Trump alipomaliza kuzungumza.
Pelosi ameichana hotuba hiyo na kusema alijaribu kutafuta kitu chochote cha kweli na cha maana kwenye hotuba hiyo na hakukiona. Tukio hilo ni mwendelezo wa mvutano kutaka Trump aondolewe madarakani.
Wasaa wa kujitapa na kujigamba
Trump ametumia sehemu kubwa ya hotuba yake kwa majigambo, ya namna alivyofanikiwa kuukarabati uchumi wa Marekani, na hadhi ya nchi hiyo, ambavyo amedai vilikuwa vimewekwa rehani na watangulizi wake.
”Miaka ya uozo wa kiuchumi imekwisha. Siku za Marekani kuhujumiwa kiuchumi na kukejliwa na mataifa mengine tumeziacha nyuma. Tumeipa pia kisogo mienendo ya kuvunja ahadi, na kutafuta visingizio vya kumomonyoka kwa uchumi, nguvu na fahari ya Marekani,” amesema Trump na kuongeza kuwa kwa miaka mitatu tu, ”tumevunjilia mbali mienendohiyo na mitazamo Marekani inadidimia.”
Masuala mengine aliyoyamulika Trump katika hotuba yake, ni mikubaliano ya kibiashara kati ya China, na mengine ya eneo huria la kibiashara katika nchi za Amerika Kaskazini, akisema hayo ni mafanikio makubwa ambayo yatarejesha maelfu ya viwanda nchini Marekani.
Amezungumzia pia sera za kupunguza kodi na kumaliza kuhusika kwa majeshi ya Marekani katika mizozo ya Mashariki ya Kati, kama ushahidi wa kutimiza ahadi alizozitoa kwa wapiga kura.
Ufa mpana kati ya vyama vya Republican na Democrat
Hotuba yake ilishangiliwa mara kwa mara na wabunge wa chama chake cha Republican waliosimama kumpigia makofi, huku wademocrat wakibakia katika viti vyao, baadhi wakizomea, na wengine hata kutoka nje.
Trump ambaye baadaye leo anatarajiwa kuondolewa hatia katika kesi anayoshtakiwa na chama cha Democrat kwa tuhuma za matumizi mabaya ya wadhfa wake, hata mara moja hakuitaja kesi hiyo katika hotuba yake.
Wakati huo huo, matokeo ya uchaguzi wa kwanza wa mchujo katika chama cha Democratic uliofanyika katika jimbo la Iowa yametangazwa, baada ya kucheleweshwa kutokana na hitilafu za kiufundi.
Baada ya kuhesabiwa asilimia 62 ya kura, meya wa zamani, Pete Buttigieg, ameshika nafasi ya kwanza, akifuatiwa na maseneta Bernie Sanders na Elizabbeth Warren, huku makamu wa rais wa zamani, Joe Biden, aliyepigiwa upatu kuongoza katika mbio za kukiwakilisha chama chake katika uchaguzi wa rais ujao, akitupwa mbali katika nafasi ya nne.


