BILA kificho, Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa amesema kuwa kasi waliyoionyesha kipindi cha pili kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba, ndiyo watakayoanza nayo Machi 8, mwaka huu watakapombana tena.
Uamuzi huo ni katika kuibadilishia mbinu Simba tofauti na ilivyokuwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza ambao Simba ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-0, Yanga ikasawazisha na matokeo mwisho kuwa 2-2.
Katika mchezo huo wa kwanza, Yanga iliingia kwa kuisoma kwa Simba, wapinzani wao wakatumia vizuri nafasi na kufunga mabao mawili, kabla ya Yanga kutumia dakika nne kipindi cha pili kufunga mabao yao dakika ya 49 na 53.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mkwasa alisema watani wao hao wa jadi ni wepesi hasa kipindi cha pili baada ya kuwaona katika mchezo uliopita waliotumia dakika nne za kipindi cha pili kurudisha mabao waliyofungwa.
Mkwasa alisema kuwa wapinzani wao hawana pumzi za kutosha, hivyo watatumia udhaifu wao kwa kuhakikisha wanashambulia kwa kasi katika vipindi vyote viwili ili kuwachosha viungo wao.
Aliongeza kuwa, mashabiki wa Yanga wasiogope kujitokeza uwanjani katika mchezo huo, kwani yeye kwa kushirikiana na kocha mkuu, Mbelgiji, Luc Eymael anaamini watapata matokeo mazuri ya ushindi katika pambano hilo.
“Kile tulichowafanya katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi ni kidogo, tumepanga kuwapa ‘sapraizi’ ya kutosha watani wetu Simba ambayo hawataamini mara baada ya kipyenga cha mwisho.
“Ninafahamu udhaifu wao wote, wala mashabiki wa Yanga wasiogope kuja uwanjani, kama unakumbuka viongozi wa Simba walivyoshindwa kunyanyuka kwenye viti vyao majukwaani baada ya mchezo uliopita wa mzunguko wa kwanza, basi safari hii itakuwa zaidi, nakuahidi hilo.
“Mimi ninawajua vizuri Simba udhaifu wao, ninaongea hivi siyo kama nawatisha bali ninamaanisha, kwa upande wa benchi la ufundi na wachezaji wala hatuhofii mchezo huo, tupo tayari kucheza nao hata kama leo,” alisema Mkwasa huku akijitanua.
STORI NA WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA

