KOCHA Mbelgiji wa Simba, Sven Vandenbroeck, ameiweka kiporo Yanga baada ya kusema mawazo yake kwa sasa ni kupata pointi sita kwenye mechi yake ya leo Jumapili dhidi ya KMC, kisha dhidi ya Azam FC Jumatano ijayo, kabla ya kuvaana na Yanga.
Mbelgiji huyo amebainisha kwamba hawezi kuiweka akilini mechi yake na Yanga kwa sababu iko mbali na kuna mechi ambazo anatakiwa azicheze kabla ya kukutana na watani zao wa jadi.
Kocha huyo kwa mara ya pili atakutana na Yanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar, Machi 8, mwaka huu baada ya ile ya awali iliyochezwa Januari 4, mwaka huu kumalizika kwa sare ya 2-2.
Sven ameliambia Spoti Xtra, kuwa kilichopo mbele yake ni mechi hizo mbili za KMC na Azam kuona watafanyaje kupata pointi na siyo Yanga.
“Kilichopo mbele yangu kwa sasa ni mechi ya kwanza na KMC (leo Jumapili) kisha Azam FC. Ninataka kuona tunapambana kupata pointi tatu kwenye mechi hizo mbili kwanza kwa sababu ndiyo ziko karibu yetu.
“Tukimaliza ndiyo tutakuwa na muda sasa wa kuanza kuangalia mechi yetu na Yanga ila kwa sasa mawazo yangu haypo kabisa katika mechi hiyo,” alisema Sven.
Katika hatua nyingine, kocha huyo ambaye anapambana kuona Simba inatetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, amesema Yanga haiwezi kuwazuia kufikia malengo yao, hivyo kila anayekuja mbele yao ni kipigo tu kuanzia sasa.
Kabla ya mechi za jana Jumamosi, msimamo wa Ligi Kuu Bara ulikuwa ukionyesha kwamba Simba inaongoza ikiwa na pointi 62, ikifuatiwa na Azam yenye 45, Namungo (43) na Yanga (41).

