×

Bocco Atuma Salamu Azam, Yanga SC

SHAMBULIAJI mkongwe na nahodha wa Simba, John Bocco, amesema ameuweka pembeni mchezo wao wa watani wa jadi dhidi ya Yanga huku akitaka kwanza wamalizane na Azam leo.

 

Simba na Azam watavaana leo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kwenye Dimba la Taifa.

Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa dabi ya Kariakoo itakayopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam itakayowakutanisha Yanga dhidi ya Simba.

Akizungumza na Championi Jumatano, Bocco alisema wanauheshimu mchezo huo wa watani wa jadi, lakini kwa hivi sasa nguvu na akili zao wamezielekeza katika pambano lao dhidi ya Azam.

 

Aliongeza kuwa ushindi dhidi ya Azam utawaongezea nguvu, morali na hali ya kujiamini wachezaji katika kuelekea mchezo wao na Yanga ambao ni lazima wawafunge baada ya kuwakosa katika mzunguko wa kwanza.

“Ushindi tunaopata unatuongezea hali ya kujiamini kuelekea michezo yetu iliyopo mbele yetu dhidi ya Azam na Yanga ambayo yote ni muhimu kwetu kupata ushindi ili tujiweke katika mazingira mazuri ya kuchukua ubingwa wa ligi.

 

“Tuna nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa baada ya kuwapita wapinzani wetu Azam na Yanga kwa idadi kubwa ya pointi, lakini ni lazima tushinde michezo yote inayofuata kwa kuanza na Azam kabla ya kukutana na Yanga,” alisema Bocco.

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave a Comment