×

Morogoro, Chimbuko Mama la Singeli

TAREHE 29.02.2020 tamasha kubwa la muziki lijulikanalo kama Mzikimnene linaloandaliwa na kituo cha redio (EFM), lilifanyika Mkoa wa Morogoro.

 

Tamasha la Mzikimnene ni moja ya matamasha makubwa sana Tanzania yanayo ibua vipaji mbalimbali hususani Singeli, huku likizidi kuangazia fursa za kiuchumi na kibiashara katika maeneo mbalimbali linapofanyika.

 

Kwa kupitia tamasha la Mzikimnene, mkoa wa Morogoro umeweza kudhihirisha vipaji vikubwa sana vya Muziki ujulikanao kama Singeli wenye mahadhi ya mdundiko pamoja na mchiriku.

Hii ilidhihirishwa kwa kupitia muamko mkubwa sana wa vijana zaidi ya 70 waliojitokeza kushindana katika kinyang’anyiro cha kuwatafuta wakali wa Singeli kwenye vipengele vya Singeli Michano na Singeli Ladha.

 

Meneja matukio kutoka efm redio (Jesca Mwanyika)  alihojiwa na kusema kwamba, tamasha la Mziki mnene linazunguka mikoa mbalimbali, lakini kwa mkoa wa Morogoro kumekuwa na muamko mkubwa sana wa vijana katika ushiriki wa mashindano haya ya kusaka vipaji vya Singeli.

 

Katika mashindano hayo waliweza kuibuka washindi wawili Phocus G Msangi jina la usanii (Mc Sinajina) ambaye alishinda upande wa Singeli Michano na Abuu Ridhiwan aliyeshinda upande wa Singeli Ladha.

Washindi hao walihojiwa na kukiri kwamba licha ya ushindi walioweza kuupata, lakini kulikuwa na mchuano mkali sana ambapo kila mshiriki alijaribu kuonyesha kipaji chake japo wao waliweza kushinda kutokana na kura za mashabiki.

 

Tamasha la Mzikimnene kupitia mashindano ya kusaka vipaji vya Singeli (Singeli Michano) limeweza kuibua wasanii wakubwa sana wanaofanya vizuri katika Muziki wa Singeli kama Jaguar, P.K, Vairas, Yuda msaliti, Segumbo na wengine wengi ambao wamekuwa wakifanya vizuri katika tasnia ya mziki wa Singeli huku wengi wakiweka matazamio na jitihada za kufika mbali.

 

Na mwandishi wako,

Andrew Sengenge.

 

Leave a Comment