BAADA ya hivi karibuni kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude kumkera Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije kwa utovu wa nidhamu, juzi Jumatano ametoa kali ya mwaka katika mazoezi ya Simba.
Hivi karibuni Mkude aliitwa katika kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Chan na kufuzu Afcon lakini hakutokea katika mazoezi hayo mpaka kambi ya timu hiyo ilipovunjwa kutokana na tishio la Virusi vya Corona.
Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kwamba juzi Jumatano, Mkude aliibuka katika mazoezi ya Simba akiwa pamoja na wachezaji wenzake waliokuwa katika kikosi cha Stars huku naye akijifanya kuwa alikuwa kwenye kambi hiyo.
Jambo hilo liliwashangaza vilivyo wachezaji wenzake hao na kumwona kama kituko katika mazoezi hayo licha ya yeye kuonekana kutokujali chochote.
Akizungumza na Championi Ijumaa, mmoja wa wachezaji wa Simba ambaye aliomba kutotajwa
jina lake alisema kuwa: “Mkude alitushangaza sana kwani hatukutegemea kama naye angejiunga na timu leo (juzi).
“Wakati tulipokuwa katika kikosi cha Taifa Stars, kila alipokuwa akipigiwa simu alikuwa akimdanganya kocha, kuwa yupo Morogoro ana matatizo ya kifamilia kumbe alikuwa hapahapa Dar, hakika tulimshangaa sana jamaa yetu huyo.”
Alipotafutwa Mkude ili aweze kuzungumzia hilo hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa.


