IDADI ya wagonjwa wa virusi vya corona nchini Uganda imeongezeka kwa kasi huku nchi hiyo ikipambana kuzuia maambukizi zaidi. Uganda imetangaza kuwa na wagonjwa wapya wanane na kufikisha idadi ya wagonjwa tisa wa virusi hivyo.
Wagonjwa hao wapya wanane wote ni raia wa Uganda ambao wamerejea nchini humo kutokea Dubai baina ya Machi 20 na 22 mwaka huu.
Waziri wa Afya wa Uganda, Jane Ruth Aceng amewaambia wanahabari kuwa kufikia sasa nchi hiyo imebaini wasafiri 2,661 wakiwemo raia wa nchi hiyo ambao wanaweza kuwa na hatari ya kusambaza maambukizi na watu wote hao wapo chini ya uangalizi maaalumu.
Wakati huohuo, wagonjwa wapya wa virusi vya corona 17 wametangazwa jana usiku nchini Rwanda na kufanya idadi ya maambukizi nchini humo kufikia watu 36.
