WAKATI uongozi wa Yanga ukidaiwa kumalizana na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo msimu uliopita wa 2018/19, Mkongomani, Heritier Makambo, tayari amekabidhiwa mtihani mzito ndani ya klabu hiyo.
Mtihani aliopewa ni wa kuhakikisha anaiongoza Yanga kuvunja rekodi yake ya kufunga mabao mengi zaidi katika michuano ya Ligi Kuu Bara iliyoiweka msimu wa 2015/16 wakati safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, ikiundwa na Mrundi, Amisi Tambwe pamoja na Mzimbabwe, Donald Ngoma.
Msimu huo ambao Yanga ilikuwa bingwa wa ligi kuu, ilifunga mabao 70, huku Tambwe pekee akifunga mabao 21 na kuwa mfungaji bora wakati Ngoma alifunga mabao 17.
Yanga kupitia kwa wadhamini wa timu hiyo, Kampuni ya GSM, inadaiwa kumalizana na Makambo na kilichobakia sasa ni kampuni hiyo kumalizana na uongozi wa timu ya Horoya Athletic ya nchini Guinea ambayo mchezaji huyo anaitumikia kwa sasa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, alisema kuwa usajili huo wa Makambo ni moja kati ya usajili bora ambao utakuwa umefanywa na timu hiyo katika kuhakikisha msimu ujao inakuwa moto wa kuotea mbali.
Alisema pamoja na kusajiliwa kwake Yanga kwa mara nyingine tena, Makambo anatakiwa kuhakikisha anaiongoza timu hiyo kuvunja rekodi ya msimu wa 2015/16 kwa kuzifumania nyavu.
“Msimu huo tulifunga jumla ya bao 70, lakini mabao 53 kati ya hayo tuliyafunga wachezaji tuliokuwa tukiunda safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
“Mimi milifunga 21, Ngoma (17), Simon Msuva (9), Paul Nonga (5) pamoja na Anthon Matheo (1).
“Kwa hiyo Makambo naye anatakiwa kuiongoza safu hiyo kama usajili wake wa kutua Yanga utakamilika kama nilivyofanya mimi nilipokuwa nikishirikiana vizuri pamoja na washambuliaji wenzangu hao,” alisema Tambwe.
SWEETBERT LUKONGE, Dar es Salaam
