×

Ishu ya Tchetche Simba ni Hivi

KUMBE Simba imeshindwa kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Muivory Coast, Kipre Tchetche kwa sababu ya dau la dola 300,000 (zaidi ya Sh milioni 692).

Hivi karibuni, katika dirisha dogo la usajili, uongozi wa Simba ulidaiwa kuwa katika harakati za kutaka kumsajili Tchetche, kwa ajili ya kuiongezea nguvu safu yake ya ushambuliaji.

 

Hata hivyo, usajili huo uligonga mwamba baada ya timu hiyo kugoma kumpatia mshahara wa dola 8,000 (zaidi ya Sh 18 milioni) kwa mwezi, lakini hivi karibuni uongozi unadaiwa kurudi tena kwa mchezaji huyo kwa ajili ya mazungumzo ya kutaka kumsajili kwa ajili ya msimu ujao.

 

Lakini kwa mara nyingine mambo yameiendea ndivyo isivyo klabu hiyo, baada ya kuona itashindwa kumng’oa katika timu ya Kedah ya nchini Malaysia, baada ya kugundua alisajiliwa kwa dau la dola 300,000 ambalo Simba wakitajiwa na klabu hiyo watashindwa kuzitoa huku nyota huyo akiendelea kuwa msaada mkubwa kwa Kedah ambayo alijiunga nayo mwaka huu akitokea Terengganu ambayo pia ni ya Malaysia.

 

Mmoja wa viongozi wa Simba ameliambia Championi Jumatatu kuwa wamegundua Tchetche alijiunga Kedah kwa kitita cha dola 300,000 (zaidi ya Sh 692 milioni) lakini pia kwa mwezi analipwa mshahara wa dola 10,000 (zaidi ya Sh 23 milioni), hivyo ni ngumu kumng’oa.

 

“Kwa hiyo ishu ya kumsajili Tchetche haipo tena, tumeachana nayo baada ya kugundua alisajiliwa na timu ya Kedah ya Malaysia kwa dau kubwa kuliko ambalo tulitaka kumpatia sisi lakini tukawa tunavutana naye na zaidi ilikuwa ni fedha ya mshahara.

 

“Dau la usajili tulilokuwa tumepanga kumpatia lilikuwa dola 100,000 (zaidi ya Sh 230 milioni) ambalo alikuwa amekubaliana nalo lakini ishu ya mshahara ndiyo ilikuwa kikwazo, yeye alikuwa anataka kwa mwezi tumpatie mshahara wa dola 8,000 (zaidi ya Sh 18 milioni) lakini sisi hatukuwa tayari kutoa kiasi hicho, jambo lililosababisha mvutano mkubwa na kujikuta tukimkosa katika dirisha dogo la usajili.

 

“Baada ya hapo tulianza tena mazungumzo naye ya kumsajili lakini mambo hayakuwa sawa na mwisho wa siku aliamua kubakia Malaysia ambako tumeona amepata dau zuri,” kilisema chanzo hicho cha habari.

 

Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ili azungumzie hilo, hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa. Picha ndogo mbele inamuonyesha Tchetche akisajiliwa na Kedah ya Malaysia.

 

SWEETBERT LUKONGE, Dar es Salaam

Leave a Comment