×

Corona: Waziri Ummy Awapa Maagizo Viongozi wa Dini – Video

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu leo Aprili 09 ametoa rai kwa viongozi wa dini nchini kuhakikisha wanaepuka misongamano kwenye nyumba za ibada hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

 

Waziri Ummy amewaomba viongozi hao kuhakikisha waumini wenye dalili za kikohozi, mafua na homa wanabaki nyumbani.

 

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wahabari jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Aprili 9, wakati wa kikao cha kitaifa cha viongozi wa dini kilichozungumzia jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

 

Amesema hadi sasa kuna idadi ya wagonjwa 25 na taarifa nyingine ataitoa mchana baada ya kupata maelezo watalaamu waliopo maabara.

 

“Ugonjwa tumeletewa kutoka nje, hivi sasa takwimu za jana, juzi na wiki iliyopita tumeanza kuambukizana wenyewe kwa wenyewe. viongozi wangu wa dini naomba niliweke wazi its no longer imported cases, tumeanza local transmission.

 

“Ndani ya siku chache tutaingia katika community transmission. Maana yake tutapata mgonjwa ambaye hajui ugonjwa ameupata wapi? Sasa hivi amekuja mtu anamuambikiza fulani ndio maana tunafanya contact (muingiliano) kujua. Bado tunatakiwa kuchukua tahadhari na kuongeza juhudi za kukabiliana na ugonjwa huu,” amesema Ummy.

 

Amefafanua kuwa hatua ya maambukizi katika jamii ni ngumu aliyeambukizwa amepewa na nani na kwamba ndani ya siku chache inawezekana tukaingia katika hatua hiyo.

 

Waziri Ummy amesema, tafiti zinaonesha virusi vya corona pia vinaambukizwa kwa njia ya hewa hivyo baada siku chache Serikali itatoa mwongozo ikiwa ni pamoja na kumtaka kila mtu anapotoka nyumbani awe amevaa barakoa ili kupunguza kasi ya mambukizi.

 

Waziri huyo amesema ni wajibu wa kila kiongozi wa dini kuhakikisha wanaendesha ibada katika utaratibu na mazingira yasiyo hatarishi ili kujikinga dhidi ya virusi vya corona, akisema makongamano ya dini sio muhimu kwa wakati huu.

 

“Ni mategemeo yetu viongozi wa dini kuepuka mikusanyiko ya watu wengi, tunategemea kupata ushirikiano wenu kuhakikisha kuwa ibada zinaendeshwa katika mazingira ambayo si hatarishi, rais ameeleza kuwa serikali haitafunga nyumba za ibada lakini ni wajibu wetu kuangalia sasa tutafanya ibada kwa namna ambayo si hatarishi kwetu na kwa waumini.

 

“Kingine tunachoomba ni kuwepo utaratibu wa kupunguza waumini wakati wa kutoka na kuingia katika nyumba za ibada, kuwa na ibada fupifupi zinazofanyika mara kwa mara, kufanya usafi wa mara kwa mara kwenye nyumba za ibada na utakasishaji,” amesema.

 

Leave a Comment