ALIYEWAHI kuwa mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, raia wa Burundi, Amissi Tambwe amesema kuwa ana hofu kubwa ya rekodi yake ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili ikavunjwa na mshambuliaji wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere.
Kagere ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa ligi kuu akiwa amefunga mabao 23, pia msimu huu anatarajiwa kuibuka mfungaji bora ambapo mpaka sasa anaongoza kwa kufunga akiwa na mabao 19 wakati wanaofuatia wakiwa na mabao 11.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Tambwe ambaye alikuwa mfungaji bora wa ligi kuu mara mbili, msimu wa 2013/14 na 2015/16 alisema kuwa anahofia rekodi yake hiyo kuvunjwa na Kagere ambaye sasa yupo kwao Rwanda alipoenda kwa ajili ya mapumziko baada ya ligi kuu kusimama kutokana na ugonjwa wa Corona.
“Kagere kusema kweli siyo mtu mzuri kabisa kutokana na kasi yake ya kuzifumania nyavu, kwa jina jingine unaweza kumuita kuwa ni moto wa kuotea mbali.
“Ananiogopesha kwani ninaona anaenda kuvunja rekodi yangu ya kuibuka mfungaji bora mara mbili katika ligi kuu ambayo nilikuwa nikiishilia, kusema kweli jamaa ananitisha,” alisema Tambwe.
SWEETBERT LUKONGE, Dar es Salaam
