WAKATI familia mbalimbali za Kikristo duniani zikisherehekea sikukuu ya kufufuka kwa Yesu Kristo, familia ya Subira Rashid (43), mkazi wa Kinondoni-Moscow jijini Dar imekumbwa na simanzi nzito.
Familia hiyo inadai Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, limesababisha kifo cha mtoto wao. Subira ambaye ni mama wa marehemu Cloud Manda (20), alidai mwanawe huyo alifariki dunia kutokana na kipigo cha Polisi.
SIMULIZI
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kuhusu tukio hilo, Subira alisema kuwa, Aprili 5, mwaka huu alipigiwa simu na jirani yake na kuambiwa kuwa, mwanawe amekamatwa na Polisi walioambatana na sungusungu maeneo hayo wanayoishi (Kinondoni-Moscow).
Alisema jirani huyo alimwambia mwanawe amekamatwa pamoja na vijana wengine na kupelekwa kituo kidogo cha polisi kilichopo maeneo ya Hananasif, Kinondoni. Akifafanua kwa kina kuhusu tukio hilo, mama huyo alisema wakati akielekea kituoni hapo, alisikia vijana hao wakipiga mayowe kufuatia kipigo kikali walichokuwa wakipewa.
Alisema baada ya kufika kituoni hapo, alimkuta mwanawe amepoteza fahamu huku wenzake kama sita wakiwa wamevimba na kutokwa damu sehemu mbalimbali.
“Niliwauliza wale Polisi alichofanya mwanangu, wakanijibu ni mhalifu… nikawaambia hata kama ni mhalifu, ni bora wangempeleka mahakamani, lakini siyo kumtesa vile. “Wakati nikiwaambia hivyo, kuna askari mmoja alikuwa akiwaambia wenzake eti mwanangu alikuwa akijifanya amezimia,” alisema.
Alisema baada ya muda, Polisi walimchukua yeye, mwanawe na vijana wengine ambapo vijana hao waliwapeleka Kituo cha Polisi cha Mwinjuma. “Mimi na mwanangu walitupeleka Hospitali ya Mwananyamala huku akiwa hajitambui na kuingizwa katika chumba cha matibabu.
“Askari ndiyo waliokuwa wakiongea na madaktari muda wote. Baada ya muda niliambiwa mwanangu amefariki dunia, yaani inaniuma sana!” Alisema mama huyo huku akilengwalengwa na machozi na kuongeza; “Polisi wamemuua mwanangu bila hatia!”
BABA MDOGO
Baada ya mama huyo kuelezea dukuduku lake, baba mdogo wa marehemu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Isdori Manda, aliongeza kuwa kifo cha Cloud kina utata. “Kwa sababu saa chache kabla ya kukamatwa, nilikuwa naye nyumbani akinisaidia kupakia mizigo kwenye gari, lakini muda mfupi baadaye nikapigiwa simu kuwa mwanangu amepigwa na Polisi na sungusungu ambao waliwavamia ndani akiwa kwenye chumba cha rafiki yake.
“Nilishangaa sana maana nilijua kama ni uhalifu, huwenda wangeniambia wamemkuta eneo la tukio, lakini wao inasemekana walikuwa vijana kama sita wamejichangisha pesa zao wanasonga ugali wale.
“Nilipohoji zaidi sababu ya kukutwa wakipika ugali ndiyo wakamatwe na kupigwa, wengine wakaniambia inasemekana walikutwa wakivuta bangi humo ndani na walikutwa na visu vitatu.
“Hata hivyo, bado niliendelea kushangaa kwa kuwa chumbani kukutwa na visu hata vitano bado siyo kosa kwa kuwa kwanza walikuwa wakipika, hivyo huwenda hivyo visu ni kwa ajili ya kukatia mboga na matumizi mengine.
“Na hata hiyo bangi kwani mtu akikutwa na bangi hukumu yake ndiyo kupigwa mpaka kufa? Mbona kuna kesi mpaka za Cocaine na marobota ya bangi zipo mahakamani na watuhumiwa hawauawi, iweje kwa mwanangu?” Alihoji baba mdogo huyo wa marehemu.
POLISI WAFUNGUKA
Kufuatia sakata hilo, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilizungumza na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, (SACP) Edward Bukombe ili alielezee tukio hilo ambapo alisema;
“Ndugu mwandishi hiyo habari hata mimi nimepata taarifa za kuambiwa kama wewe, ila ninachoweza kukuambia ni kwamba tuko kwenye uchunguzi wa tukio hilo,” alisema Kamanda Bukombe.
Kuhusu kushikiliwa kwa Polisi wanaohusika na tukio hilo, Kamanda Bukombe alisema kuna watu kadhaa wanaohojiwa, lakini hakupenda kuweka bayana zaidi suala hilo.
“Suala hili bado lipo kwenye uchunguzi, kuanza kuweka wazi kinachoendelea ni kuharibu mwenendo wa uchunguzi,” alisema Kamanda Bukombe. Marehemu alizikwa Makaburi ya Kinondoni, Mwembe-Jini, Aprili 8, mwaka huu.
STORI: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN, DARMmoja wao alifariki Aprili 11.

