×

Afrika Inaweza Kuwa Kitovu Kipya cha Corona – WHO

AFRIKA huenda ikawa kitovu kipya cha mlipuko wa virusi vya corona, Shirika la Afya duniani (WHO) limeonya kutokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa la visa vya ugonjwa huo wiki iliopita barani humo.

Kumekuwa na zaidi ya visa 1,000 na zaidi ya maambukizi 18,000 kote barani Afrika kufikia sasa ijapokuwa viwango hivyo viko chini zaidi ya vile vinavyoonekana katika baadhi ya mataifa ya Ulaya na Marekani.

WHO linasema kwamba virusi hivyo vinaonekana kusambaa katika maeneo ya mashambani pia ambako bara hilo  halina ,mashine za kutosha za kuwasaidia wagonjwa kupumua ili kukabiliana na mlipuko huo.

Mkurugunzi wa shirika hilo barani Afrika, Dkt Matchidizo Moeti, aliliambia shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) kwamba shirika hilo limeshuhudia kuenea kwa virusi hivyo kutoka miji mikuu hadi mashambani katika mataifa ya Afrika Kusini, Nigeria, Ivory Coast , Cameroon na Ghana.

Amesema kwamba kwa sasa wanaangazia kuzuia badala ya kutibu virusi hivyo kwa sababu mataifa ya Afrika hayana uwezo kuwatibu wagonjwa wengi wa virusi vya corona.

”Tunataka kupunguza kiwango cha watu ambao wanafikia kiwango cha kuhitaji mashine za kuwasaidia kupumua katika chumba cha wagonjwa mahututi  kwasababu tunajua kwamba vifaa hivi ni vichache kwa kiwango chochote miongoni mwa mataifa mengi ya Afrika,” alisema na kuongeza:

“Nataka kusema kwamba suala la mashine za kusaidia watu kupumua ni mojawapo ya changamoto kubwa ambazo mataifa hayo yanakabiliana nayo.”

Kwa wagonjwa walio katika hali mabaya zaidi wakiugua ugonjwa wa corona, upatikanaji wa mashine za kuwasaidia kupumua unaweza kuwa changamoto kubwa

Mashine hizo zinasaidia mapafu kupumua na kutoa hewa chafu ya kaboni mwilini wakati mtu ni mgonjwa sana, hali ya kwamba hawezi kujisadia kupumua.

Mojawapo ya vifo vilivyorekodiwa kutokana na virusi vya corona barani Afrika ni mwandishi wa Zimbabwe, Zororo Makamba, mwezi Machi mwaka huu.

Halmashauri ya Jiji la Harare imesema  halina mashine za kupumulia  na kuna hofu kwamba ugonjwa huo unaweza kusambaa haraka katika maeneo ya watu wengi ambapo mtu hawezi kufuata agizo la kutokaribiana na watu wengine ambapo wengi hawana uwezo wa kupata maji safi na sabuni.

Leave a Comment