IDADI ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini Kenya imeongezeka hadi 281 baada ya visa vingine 11 kuthibitishwa leo Jumatatu, Aprili 20, 2020. Watano kati ya wagonjwa hao 11 ni wanawake na wanaume 6. Wagonjwa wote wana umri kati ya miaka 11 na 80.
Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe amesema wagonjwa wapya saba wameripotiwa mjini Mombasa pwani ya Kenya huku wanne wakitokea jijini Nairobi. Wagonjwa wawili wamepona na kuruhusiwa kuenda nyumbani na kuongeza idadi ya waliopona ugonjwa huo nchini Kenya kufikia 69.
Vifo vilivyotokana na ugonjwa wa corona nchini humo bado ni 14. Waziri Kagwe pia amethibitisha kuwa jumla ya watu 455 wamekamatwa na kuwekwa karantini ya lazima kwa kukiuka masharti ya kafyu iliyowekwa kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.
Serikali ilikuwa imetoa onyo kwamba watakaokiuka kafyu watawekwa karantini ya lazima kwa gharama yao baada ya visa vya watu kukamatwa kwenye baa na hafla za nyumbani kuongezeka.
Pia, kumekuwa na madai ya watu kutoa hongo kwa polisi ili kupita vizuizi na kuingia aukutoka miji iliyowekewa marufuku ya usafiri kama vile Nairobi. Kenya ina jumla ya vituo 33 vya karantini vinavyowazuilia watu 483 kwa sasa.
