×

Winga Mkongo: Nimezungumza Nayanga SC, Nakuja Bongo

AMEKUBALI kutua Yanga! Ndio kauli ambayo imetolewa na winga machachari, Tuisila Kisinda anayekipiga katika timu ya AS Vita ya nchini DR Congo.Tuisila mwenye umri wa miaka 20, amekuwa muhimili mkubwa ndani ya timu hiyo tangu asajiliwe mwanzoni wa mwaka 2019, akitokea AS Maniema.

 

Winga huyo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana, alifanikiwa kuifunga Simba bao moja katika ushindi wa mabao 5-0 walioupata AS Vita hatua ya makundi.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, moja kwa moja kutoka DR Congo, Kisinda alisema kuwa tayari ameanza kufanya mazungumzo na viongozi wa Yanga juu ya yeye kutua ndani ya timu hiyo huku akisema japo mambo bado hayajakamilika lakini yupo tayari kuitumikia klabu hiyo ambayo anaamini ni moja ya klabu kubwa Afrika.

 

“Tayari nipo kwenye mazungumzo na viongozi wa Yanga, mazungumzo yetu bado hayajakamilika, nadhani kutokana na hali halisi ya kidunia ilivyo kwa sasa lakini kama mazungumzo yatakuwa mazuri basi nitakuja kuicheza Yanga.

 

“Yanga ni kubwa na nzuri kwa Afrika, nimeifuatilia kwa kuwa ni maarufu kwa Ukanda wa Afrika Mashariki pia ina wachezaji wengi wazuri ambao wanacheza pale,” alisema mchezaji huyo.

 

Kisinda licha ya kuwa na uwezo wa kucheza winga ya kulia, pia hucheza katika baadhi ya maeneo kama winga wa kushoto, kiungo mshambuliaji na mshambuliaji wa kati.

 

Hivi karibuni kabla ya kuibuka kwa janga la Corona, iliripotiwa kwamba, mabosi wa Yanga chini ya wadhamini wao GSM, walitua DR Congo kufanikisha usajili wa winga huyo, lakini hadi sasa mambo hayajakamilika.

STORI: MARCO MZUMBE, DAR

Leave a Comment