
DAR: Kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kimeibua mshtuko ndani ya Burundi, Afrika na dunia kwa ujumla kutokana na nyakati muhimu ambazo Taifa hilo linapitia.
Kifo chake ambacho kimeacha simanzi kwa Warundi na watu wa kada mbalimbali, pia kimeibua utata kutokana na taarifa za madai kuwa amefariki kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona hasa ikizingatiwa mkewe anatibiwa nchini Kenya, pia ameambukizwa Corona.
Hata hivyo, Msemaji wa Serikali, Balozi Willy Nyamitwe, amekanusha madai ya Corona kuhusu Nkurunziza na kubainisha kuwa rais huyo aliyeaga dunia Juni 9 mwaka huu, alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya moyo.
Mbali na hayo, Rais Pierre Nkurunziza ambaye alitarajiwa kukabidhi madaraka Agosti mwaka huu baada ya Evariste Ndayishimiye kushinda kiti cha urais katika uchaguzi wa Mei mwaka huu, ni kiongozi aliyeacha historia ya kipekee ndani na nje ya nchi hiyo.
Historia hiyo inabainisha namna kiongozi huyo alivyopanda na kushuka katika kipindi cha uongozi wake ambao ulikuwa ukingoni kabisa kupitia chama cha CNDD –FDD.
KUPANDA
Amani; Licha ya taifa hilo kukumbwa na misukosuko ya uvunjifu wa amani katika kipindi chake, Rais Nkurunziza ambaye aliingia madarakani kwa mara ya kwanza 2005, alifanikiwa kuivusha nchi hiyo katika misukosuko hiyo.
Awali, itakumbukwa kuwa taifa hilo lilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha mauaji ya watu 300,000.
Hata hivyo, mwaka 2015 juhudi zake ziliingiwa na doa baada ya wapinzani kupinga rais huyo kugombea muhula wa tatu, hali iliyosababisha machafuko yaliyogharimu maisha ya watu zaidi ya 100 huku 150,000 wakiikimbia nchi yao.
Aidha, alifanikiwa kuirejesha Burundi kwenye amani, hali ambayo sasa imedhihirika hata kwa nchi jirani ikiwamo Tanzania ambayo mara kwa mara imekuwa ikiwarejesha wakimbizi wa Burundi nchini humo.
Umoja; Katika kujenga umoja wa kitaifa, pia Rais huyo alifanikiwa pakubwa baada ya kutumia mbinu mbalimbali kurejesha umoja baina ya raia wa nchi wanaotoka katika makabila makubwa ya Wahutu na Watusi.
Nkurunziza ambaye alikuwa muumini wa dhati wa dini ya Kikristo (Mlokole), alikuwa mwimbaji hodari ambaye mara kwa mara alionekana akijumuika na waimbaji nchini humo, hali iliyoamsha hamasa ya umoja wa kitaifa.
Pia Nkurunziza alikua mchezaji hodari wa mpira wa miguu na mara kwa mara alikuwa akionekana akicheza mpira na timu mbalimbali nchini humo hali ambayo iliendelea kudumisha umoja kupitia michezo.
Alikua pia kocha wa timu ya daraja la kwanza mwanzoni mwa miaka ya 1990. Na baadaye kumiliki timu ya Hallelujah ambayo alikua akishiriki kucheza mpira katika nafasi ya ushambuliaji na alikuwa akifunga mara kwa mara.
Mchamungu; Mbali na kuwa mlokole, Nkurunziza na mke wake Denise, waliwahi kuripotiwa kuwaosha miguu watu waliokuwepo kwenye mkusanyiko.
Sio tu watu ambao Nkurunziza alikua na imani kuwa wanamuamini. Bali uongozi wake pia aliamini ni kutoka kwa Mungu.
“Ana amini kuwa ni kiongozi kwa matakwa ya Mungu, na hivyo anashughulika na serikali yake katika matakwa hayo,” alisema msemaji wake Willy Nyamitwe.
Uchaguzi wa amani; Katika moja ya sifa ambayo Nkurunziza alifanikiwa, ni maamuzi ya kukubali kuachia madaraka licha ya Katiba ya nchi hiyo, kumruhusu kuwania kuongoza nchi hiyo hadi mwaka 2034.
Baada ya mabadiliko ya katiba mwaka 2015, Nkurunziza alikubali kuachia madaraka mwaka huu 2020, na kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi ambao ulifanyika kwa amani katikati ya janga la maambukizi ya Virusi vya Corona nchini humo.
KUSHUKA
Mtawala wa kiimla; Wakosoaji wake ikiwemo wapinzani kutoka vyama karibu 40 na watetezi wa haki za binadamu, wao walikuwa na mtazamo tofauti kuhusu yeye.
Walimtuhumu kuwa dikteta na ambaye hataki kuachia madaraka kutokana na kuongoza kwake kwa mihula mitatu.
Hayo pia yalisababisha kufanyika kwa jaribio la kumpindua ambalo halikufanikiwa. Mkuu wa zamani wa majeshi Godefroid Niyombare aliongoza mpango huo wa kutaka kumuondoa madarakani mwaka 2015. Baada ya kushindwa kwa mpango huo, wapinzani wakadai kuwa uchaguzi wa mwaka huo haukuwa wa uhuru wala haki.
Kuminya uhuru wa vyombo vya habari; Kiongozi huyo alikuwa akishutumiwa kuminya uhuru wa vyombo vya habari baada ya mwaka uliopita serikali yake kupiga marufuku matangazo ya BBC na Sauti ya Amerika (VOA) ambapo serikali ya Burundi ilidai yamechafua sifa ya nchi.
Mbali na vyombo hivyo vya nje, pia ndani ya nchi redio kadhaa za kibinafsi ziliharibiwa na kufungwa nchini humo wakati wa mzozo wa kisiasa uliozuka mnamo 2015, wakati rais Nkurunziza alipotangaza nia yake ya kuwania muhula wa tatu katika uchaguzi wa urais alioshinda baadaye mnamo mwaka 2015.
Kuwazuia wapinzani; Tangu alipoingia madarakani 2005, Nkurunziza ameshutumiwa kwa kuminya uhuru wa kidemokrasia nchini humo.
Hali hiyo ilisababisha takribani watu 430,000, wakiwemo wanasiasa wa upinzani kuitoroka Burundi.
Ubinafsi, kujilimbikizia mali; Wakati akielekea ukingoni mwa utawala wake, Nkurunziza alijiweka katika taswira mbaya baada ya Januari 21, mwaka huu, Bunge la Burundi kupiga kura na kupitisha kwa asilimia 98 mambo makuu manne.
Mosi, Nkurunziza kulipwa kiinua mgongo dola 530,000 (Sh1.22 bilioni) mara baada ya kuondoka madarakani.
Pili, kujilipa mshahara wa Urais maisha yake yote. Sheria kuwa mshahara huo wa milele, iliwahusu marais wastaafu watakaoingia madarakani kwa njia ya kidemokrasia.
Tatu, kujengewa makazi ya kifahari ambayo ataishi miaka yote baada ya kuondoka madarakani.
Nne, ilipitishwa kuwa baada ya Nkurunziza kuondoka madarakani, hataitwa Rais Mstaafu, bali atafahamika kama Kiongozi Mkuu wa Nchi (The Supreme Leader) au Muongozaji Mkuu (The Supreme Guide).
Aidha, Machi 2018, mabadiliko ya Katiba ya chama tawala, Burundi, CNDD-FDD, yalitambulisha cheo cha Kiongozi Mkuu wa chama na Nkurunziza alipitishwa kuwa kiongozi mkuu wa milele.
Hayo yote yalijiri wakati katiba ya Burundi ya mwaka 2005, ilipitisha cheo cha Useneta wa milele kwa wakuu wa nchi wastaafu. Nkurunziza aliona useneta ni cheo kidogo na kuamua Kiongozi Mkuu wa milele, Burundi.
NKURUNZIZA NI NANI?
Nkurunziza ambaye alizaliwa Desemba 1963, Bujumbura, Burundi, baba yake alikuwa Mhutu, Mkatoliki na mama yake, Mtutsi, Mprotestant.
Baba yake, Eustache Ngabisha, japo alikuwa Mhutu, alijiunga na chama cha Watusi cha UPRONA, akawa kiongozi, kisha akachaguliwa kuwa mbunge na baadaye Gavana wa majimbo mawili.
Ngabisha (baba wa Nkurunziza), aliuawa wakati wa mauaji ya kimbari Burundi (Wahutu na Watusi) mwaka 1972. Wakati huo Nkurunziza alikuwa na miaka tisa tu.
Nkurunziza alikuwa mwanazuoni mwenye shahada ya ualimu wa michezo na saikolojia. Alikuwa mhadhiri msaidizi wa Chuo Kikuu cha Burundi kabla ya vita ya kiraia mwaka 1993, iliyozuka baada ya kuuawa Rais Melchior Ndadaye.
Nkurunziza pia alikuwa mcheza soka mwenye kipaji. Hata hivyo, alishutumiwa kutotaka kukabwa, zaidi kuchezewa rafu akiwa mchezoni kwa sababu yeye ni Rais.
Mwaka 1995, Nkurunziza alijiunga na kikundi cha waasi cha CNDD-FDD, akapanda vyeo hadi kuwa katibu mkuu. Enzi akiwa msituni, alikoswa kuuawa mara nyingi na alihukumiwa kifo na Mahakama ya Burundi bila yeye kuwepo mahakamani. Makosa yake yalitajwa ni uhaini na mauaji.
Mwaka 2001, Nkurunziza alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CNDD-FDD. Mwaka 2003, baada ya suluhu ya mgogoro wa kisiasa Burundi kupatikana chini ya usuluhishi wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini; Nelson Mandela, Nkurunziza aliteuliwa na Rais wa mpito, Domitien Ndayizeye, kuwa Waziri wa Utawala Bora.
Mwaka 2005, Nkurunziza alichaguliwa na Bunge kuwa Rais wa Burundi, mwaka 2010 alichaguliwa muhula wa pili. Mwaka 2015, aligombea muhula wa tatu na kushinda lakini alisababisha mzozo mkubwa kwa kile kilichoonekana, aliipindua Katiba ya Burundi kugombea muhula wa tatu.
Stori: GABRIEL MUSHI, Ijumaa