
MMOJA wa warembo wanaotrendi kwenye mitandao ya kijamii (sosholaiti) kutokana na umbo lake matata, ni mwanamitindo msomi Bongo, Jacqueline Obeid almaarufu ‘Poshy Queen’.
Poshy amepata umaarufu kutokana na umbo lake hilo alilojaaliwa na Mwenyezi Mungu, lakini hivi karibuni alipotea ghafla kiasi cha watu kuuliza nini kimempata?
Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limemtafuta Poshy na kufanya naye mahojiano maalum (exclusive) ambapo amefunguka mengi ikiwemo ishu ya kuogopwa na wanaume kutokana na gharama;
IJUMAA WIKIENDA: Mambo vipi Poshy?
POSHY: Poa tu, nipo, ninapambana.
IJUMAA WIKIENDA: Siku hizi umekuwa kimya sana tofauti na zamani, nini kimetokea?
POSHY: Kiukweli nimekuwa siyo mtu wa mitandaoni, ilitokea tu watu wakaanza kunizungumzia, lakini napenda maisha ya peke yangu.
IJUMAA WIKIENDA: Kwa hiyo sasa hivi umejificha ndiyo maana hata watu hawakuzu ngumzii?
POSHY: Hapana, nipo kama kawaida. Ni kwa sababu tu siyo mtu wa kujichanganya, nafurahi sana nikiishi hivi kwani maisha yangu siyo ya mtandaoni.
IJUMAA WIKIENDA: Kuna kipindi ulifungua duka la nguo za ndani la Poshy Trends maeneo ya Sinza (Dar), lakini kwa sasa silioni, halafu nasikia watu wanasema umefulia, hii imekaaje?
POSHY: Sijafunga, nimehamia Shekilango (Dar) na uzuri limekuwa duka kubwa sana.
IJUMAA WIKIENDA: Kwa upande wako, Corona imeathiri biashara yako kwa kiasi gani?
POSHY: Sidhani kama kuna biashara imesalimika, labda ya barakoa, lakini sasa hivi Mungu ni mwema anasaidia.
IJUMAA WIKIENDA: Mwanzoni baadhi ya watu walijua huwezi biashara, kwani usingeweza kukaa mwenyewe kama ilivyo kwa mastaa wengi, wewe uliwezaje?
POSHY: Mimi kama sina kazi, napenda sana kulala. Ikifika saa 3:00 usiku nakuwa kitandani na kuamka, naamka mapema saa 12:00 alfajiri, sasa kwa nini nisiende kukaa dukani kwangu ambako ndipo ninapata pesa ya kuendeshea maisha yangu?
IJUMAA WIKIENDA: Kuna kipindi ulikuwa unaogopa kwenda hata sokoni kutokana na umbo lako, vipi sasa hivi?
POSHY: Ninachoamini kila kitu kina wakati wake kwa sababu kipindi kile ilikuwa nikiamka nipo kwenye mitandao ndiyo maana ikawa ni changamoto, lakini sasa hivi naona ni kawaida tu.
IJUMAA WIKIENDA: Wewe ni mrembo mwenye umbo matata, lakini umekuwa ni mtu wa kujishusha, tofauti na wengine, unawezaje?
POSHY: Mimi najiona kawaida, wala sitaki umaarufu wa duniani unifanye niwe kipofu.
IJUMAA WIKIENDA: Vipi kuhusu usumbufu kwa wanaume unapokuwa dukani maana najua wanakuja sana!
POSHY: Sioni kama ni usumbufu, bali ni fahari maana nafanya biashara na wateja wengi wanataka kuniona dukani. Mimi naona ni sawa tu kwa sababu ni biashara.
IJUMAA WIKIENDA: Mastaa wa kike wanapenda kuvaa mavazi ya gharama, vipi kwa upande wako mavazi yanagharimu kiasi gani?
POSHY: Napenda kuvaa vitu ambavyo vina ubora wa kutosha. Kwa mfano nikibeba begi, liwe ni begi la ukweli. Ninachoshukuru mwili wangu hauhitaji vitu vingi. Ninavaa chochote.
IJUMAA WIKIENDA: Inawezekana kuna mwanaume anataka kukuchumbia, lakini anaogopa gharama unayotumia kwenye mavazi na hata manukato. Je, nini mtazamo wako?
POSHY: (Kicheko) mwanaume mwenye nia ya kweli ya kunioa, hawezi kuhofia gharama, anatakiwa kuhofia ombi lake atalifikisha vipi kwa sababu mimi naweza kuvaa nguo ya kawaida tu, lakini gharama yake inaanzia laki mbili na kuendelea. Kuhusiana na pafyumu, napendelea za kupoa, lakini nzuri za kuanzia laki tatu hadi milioni moja.
IJUMAA WIKIENDA: Watu wengi wamekuwa na wasiwasi na umbo lako, wanadai ulifanya upasuaji, je, ni kweli?
POSHY: Unajua mtu wa pembeni anaweza kukuongelea vyovyote kwa sababu hakujui, lakini wanaokujua wananyamaza, sasa watu kama hao ni kuwaangalia tu maana kuna wengine wanajifurahisha tu. Kingine kwa nini wakereke na umbo langu?
IJUMAA WIKIENDA: Unaepukana vipi na usumbufu wa wanaume?
POSHY: Usumbufu upo kwa kila mwanamke, ni jinsi tu ya kukabiliana nao. Pia kuongea kistaarabu kwa anayekusumbua kwa sababu mwisho wa siku, wewe ni wa mtu maalum kwa aliyepangwa kwa ajili yako.
IJUMAA WIKIENDA: Je, una mchumba?
POSHY: Ninaye na tunapendana sana.
MAKALA: IMELDA MTEMA, BONGO