×

GSM Watupa Kombora Simba SC

MKURUGENZI Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, Injinia Hersi Said, amesema kuwa ni aibu kwa timu hiyo kumaliza msimu bila ya kubeba kombe, huku akiahidi kupambana kulichukua Kombe la Azam Sports Federation.

 

Kauli hiyo ni salamu tosha kwa watani wao Simba wanaotarajiwa kupambana nao kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Jumapili hii ukiwa ni mchezo wa nusu fainali.

 

Simba tayari mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na jana Jumatano walikabidhiwa kombe lao baada ya kucheza dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Said ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Usajili Yanga, alisema kuwa GSM haijawahi kushindwa, hivyo kama wadhamini watahakikisha wanafanya maandalizi makubwa ya timu yao kwa kuwafunga Simba na kuchukua kombe hilo.

Said alisema kuwa, Yanga ni kati ya klabu kubwa Afrika, hivyo ni aibu kwao kumaliza msimu huu bila ya kombe lolote, hivyo amewataka mashabiki wa timu hiyo kuungana kwa pamoja katika kuelekea mchezo wao dhidi ya Simba kwa kujitokeza uwanjani kuwasapoti wachezaji.

 

“Ni aibu kwa timu kubwa kama Yanga katika ukanda huu wa Afrika kushindwa kuchukua kombe, hivyo kama wadhamini tumepanga kufuta aibu hiyo kwa kuhakikisha tunafanya kila liwezekano lililokuwepo ndani ya uwezo wetu ili tuchukue ubingwa huu.

 

“Tumeandaa kambi nzuri na bonasi za wachezaji kuelekea mchezo ujao wa nusu fainali dhidi ya Simba, lengo ni kuwaongezea morali wachezaji ya kupambana ili malengo yetu ya kuchukua kombe hilo yatimie,” alisema Said.

STORI: WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave a Comment