
NYOTA wa Al Ahly, Walter Bwalya, amesema kuwa watakuja Dar kwa lengo moja la kusaka ushindi mbele ya Simba kwenye mchezo wao wa hatua ya makundi ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Al Ahly ambao ni wababe wa soka ndani ya Afrika, wanatarajiwa kumenyana na Simba, Uwanja wa Mkapa, Februari 23. Kwa sasa kwenye Kundi A, Simba ni vinara wakiwa na pointi tatu baada ya kufungua pazia kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Vita, mchezo uliochezwa DR Congo.
Lakini Al Ahly na Al Merrikh hawajacheza mechi yoyote na wanatarajiwa kuvaana kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Bwalya alisema kuwa wanawatambua vizuri wapinzani wao, hivyo hawatawapa shida kupata matokeo ndani ya uwanja.
“Tunawatambua Simba uimara wao na pale ambapo wanakosea, hivyo tutakuja Dar kwa lengo moja la kusaka ushindi na hilo linawezekana kwa kuwa tupo imara.
“Nitapambana nami pia kuweza kuifunga Simba ili tuweze kufanikisha malengo ya klabu ambayo ni kutwaa ubingwa wa Afrika,” alisema.
IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam