
RAIS wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga, amesema kitendo Hayati Benjamin Mkapa kukiri mambo aliyowahi kukosea wakati wa uongozi wake akiwa Mkuu wa nchi katika kitabu chake cha ‘My life, My Purpose’ ni ishara ya unyenyekevu na kumpenda Mungu.
Ametoa kauli hiyo leo wakati wa ibada ya mazishi ya kuaga mwili wa Mkapa katika jijini cha Lupaso na kuwataka watu kuishi maisha ya haki, utu na uadilifu ili kusudio la Mungu katika uumbaji lipate kutimia, kwa kuwa walipo ni wasafiri na kwamba inatupasa kuishi na kutenda mema.
“Kama mnavyoona alifanya toba ya hadhara na kuandika kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’ toba ni hujenga, uvumilivu, msamaha, kujikatalia, uwajibikaji na nyingine nyingi ambazo zimebaki kama kielelezo cha kufikia uzima wa milele,” alisisitiza.
Moja ya mambo aliyokiri kukosea katika kitabu chake hicho ni kuhusiana na suala la Jeshi la Polisi kuwavamia na kuwapiga wafuasi wa upinzani walipokuwa wakiandamana mwaka 2001 visiwani Zanzibar, jambo lililosababisha mauaji, jambo ambalo halikumfurahisha yeye wakati akiwa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema dhambi ya kutofanya kitu ndiyo inatawala dunia kwa leo, hutashitakiwa na mtu lakini hutashtakiwa kwa kutofanya lolote, na kwamba siyo kuungama kwa maneno bali kutafsiri kwa vitendo na kwa dhati tunayojifunza.
Askofu Nyaisonga, amesema Mkapa kila alipokwenda kusoma ndani na nje ya nchi alijiunga na chama cha wanafunzi Wakotoliki, jambo ambalo ni fundisho kwa watu na kwamba hakuogopwa na watu ndani na nje ya kanisa, na hakuogopwa na watu wake .