×

Bashiru: Kazi na Bata, Sijui Wanalala na Bata! – Video

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amesema anashangwazwa na kaulimbiu ya moja ya vyama vya upinzani wanaodai kuwa ‘KAZI NA BATA’ huku akieleza kutoielewa vizuri kauli hiyo iwapo watu hao wanafanya kazi pamoja na bata.

 

Amesema hayo leo Alhamisi, Agosti 6, 2020, wakati akizungumza na wafuasi wa CCM kwenye hafla ya Rais Magufuli kuchukua fomu ya kuwania tena urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muhula wa pili, hafla iliyofanyika katika makao makuu ya CCM, Dodoma.

 

“Mwaka huu wa uchaguzi, tutasikia mengi na tutakuwa na wagombea wa aina nyingi, na tutapata misamiati ya kila namna, nimeshasikia msamiati wa kazi na bata…. sijui wanafanya kazi wakiwa na bata, wakichinja bata, wakilala na bata au wanafanya kazi wakitumikisha bata.

 

“CCM siyo chama cha kufanya kazi na bata, tena bata wachafu usipokuwa makini, chama kinafanya kazi na Watanzania, uko msemo mwingine mtausikia. Kuna msemo kwamba eti utapigiwa kura na Madaraja, Ndege, Mahospitali, Vivuko, Shule na Umeme wa vijijini.

 

“Watu watakupigia kura kwa sababu vitu hivyo umevifanya kwa jasho lao. Ninachowaomba wana-CCM, tusipoteza muda na maneno ya kejeli na mizaha, sisi ni watu wa kazi na maendeleo, kuna wakati nilikuwa nafanya utani, leo natamka si utani tena, mitambo ya ushindi imewashwa rasmi.

 

“Lazima mitambo iwe na kiongozi, dereva wa kushika breki kwenye mteremko, kutokutoa rushwa kwa trafiki barabarani, siku 60 za kampeni, tunawakabidhi Umoja wa Wazazi Tanzania. Muda wa kutesti mitambo umeisha, kazi ya kutafuta kura, kuzilinda, kulinda wapiga kura, kuhamasisha wapiga kura, nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda, tunawakabidhi Umoja wa Vijana wa CCM.

 

“Ushindi wa mwaka huu ni wa kishindo kikubwa. Lakini mitambo hii ni ya kisasa, inahitaji mafuta, maji ya kupozapoza ili mwili ukipata joto, kazi hiyo ni ya kina mama wa kike, Mama (Gaudensia) Kabaka yupo hapa. Tutashinda nafasi za kutosha, tutashinda nafasi za kutosha za udiwani na kuongoza halmashauri zote nchi nzima. Tutakuwa na wingi wa wabunge wa Jamhuri ya Muungano. Tutakuwa na wawakilishi wa kutosha.

 

“Chama chetu kimekuteua kwa sababu ya uwezo wako wa kuongoza, kimekuchagua kwa sababu ya ucha Mungu wako na utii wako wa kusimamia maslahi ya Taifa. Mkutano Mkuu uliokupitisha kwa 100% umezingatia rekodi ya utumishi wako ndani ya Serikali kwa zaidi ya miaka 20. Wewe ni mtu wa watu, mnyenyekevu, kimbilio la watu, kiboko ya mafisadi na wala rushwa.

 

“Kazi ya ‘Usultani’ kwenye vyama waachie unaoshindana nao, kazi ya kubadilisha rangi ya vyama kila mwaka waachie unaoshindana nao, CCM ni chama cha uongozi, tunashindana na vyama vya uchaguzi,” amesema Bashiru.

 

Leave a Comment