JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro, linamshikilia Shinje Njilangila (30), mkazi wa Kijiji cha Mbamba, wilayani Kilosa kwa tuhuma za mauaji ya shemeji yake Dotto Ngembe (28), kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Agosti 12 baada ya Ngembe kuingilia mgogoro wa kimahusiano uliozuka baina ya mtuhumiwa na mkewe, Kulwa Ngembe, ambaye ni dada wa marehemu.
Kamanda Mtafungwa alisema mauaji hayo yalitokea nyumbani kwa marehemu ambaye alikuwa amewaita wanandoa hao kwa ajili ya kusuluhisha ugomvi uliokuwa ukiendelea baina yao, ndipo mtuhumiwa alipomshambulia shemeji yake hadi kumsababishia umauti.
“Chanzo cha tukio hili mtuhumiwa alimfuata mkewe nyumbani kwa shemeji yake kwa ajili ya usuluhishi, lakini ilipofika majira ya saa sita usiku ndipo alipofanya mauaji kwa kaka wa mke wake aliyekuwa akimtuhumu kuwa ndiyo chanzo cha mgogoro wao na baada ya kutekeleza mauaji hayo alikimbia kwenda mafichoni,” alisema Mtafungwa.
Katika tukio jingine jeshi hilo linawashikilia watu watano kwa tuhuma za wizi kwa njia ya kimtandao, walipojaribu kumtapeli Pendo Thomas (29), mfanyabiashara mkazi wa kijiji cha Dumila Juu, kata ya Dumila, Wilaya ya Kilosa pamoja na gari aina ya Toyota Carina, yenye namba za usajili T.620 BYM, walilokuwa wakisafiria.
Alisema, Julai 30, mwaka huu mfanyabiashara huyo ambaye ni wakala wa huduma za kifedha alitaka kuibiwa Sh. 300,000 na mtuhumiwa Zahura Ally (33), mkazi wa jijini Mwanza kwa kupokea ujumbe wa uongo wa simu ambao mfanyabiashara huyo aliugundua na kutoa taarifa katika vyombo vya dola.
“Tumewakamata watuhumiwa sugu wote watano wa makosa ya wizi wa njia ya mtandao ambao taarifa zao zinaonyesha wamewahi kufanya matukio haya ya wizi katika mikoa ya Rukwa, Arusha, Dodoma, Mbeya, Dar es Saalam, Shinyanga na Mwanza,” alisema Mtafungwa.
Aliwataja wengine wanaoshikiliwa katika tukio hilo ni Heri Ibrahim (30) na Yassin Juma (30), wote wakazi wa Mwanza wengine ni Isaya Erasto miaka (32), pamoja na Goodluck Richard (32), wakazi wa jijini Arusha.
Kadhalika jeshi la hilo pia limekamata mirungi mabunda 49 yenye uzito wa kilogramu 22, ambayo yalikuwa yatelekezwe kwenye pikipiki moja yenye namba MC 239 BBH, iliyokuwa inatumika kusafirisha madawa hayo.
Chanzo: IPP Media.
